1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Mashirika yafuta safari za ndege kwenda na kutoka Beirut

29 Julai 2024

Safari za ndege zimefutwa au kucheleweshwa katika uwanja wa ndege mjini Beirut nchini Lebanon wakati hali ya wasiwasi ikiongezeka kuhusu hali ya kiusalama.

https://p.dw.com/p/4irDN
Ndege aina za Airbus A 380 za Lufthansa mjini Munich
Ndege za shirika la ndege la Lufthansa katika uwanja wa ndege mjini MunichPicha: Frank Hoermann/SVEN SIMON/picture alliance

Hali hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa mivutano kati ya Israel na kundi la kisiasa la wanamgambo la Hezbollah.

Shirika la ndege la Lufthasa limefahamisha leo Jumatatu kwamba limefuta safari zake tano za kuelekea na kutoka mjini Beirut zinazohusisha mashirika yake ya ndege ya Swiss Airlines, Eurowings na Lufthansa, kwa ajili ya kuchukua tahadhari.

Soma pia: Kundi la Hezbollah ladai kuishambulia Israel kwa roketi

Mwishoni mwa wiki shambulio la roketi lilisababisha vifo vya vijana 12 na watoto katika eneo la milima ya Golan na tukio hilo limeongeza wasiwasi kwamba Israel na kundi hilo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran huenda wakaingia katika vita kamili.

Jana baraza la mawaziri linalohusika na usalama la Israel liliidhinisha serikali kujibu shambulio hilo la milima ya Golan.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW