Mashambulizi ya anga yauwa takribani watu 30 Sudan
5 Februari 2025Duru za kitabibu zimeeleza kuwa mashambulizi ya anga ya wanamgambo wa Sudan yaliyofanyika Jumanne yamewaua watu watano nje ya moja ya hospitali za mwisho zinazoendelea kuwahudumia wagonjwa kwenye mji wa Omdurman. Afisa katika hospitali ya Al-Nao ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, amesema wafanyakazi wa kujitolea ni miongoni mwa watu waliouawa.
Kwa mujibu wa afisa huyo, mabomu yaliangukia katika bustani iliyo karibu na hospitali hiyo, huku wakilitupia lawama kundi la wanamgambo wa RSF kuhusika na mauaji hayo. Hospitali ya Al-Nao, ambayo inapata msaada kutoka kwa Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, iko kwenye eneo linalodhibitiwa na jeshi la Sudan, na imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara tangu vita vilipozuka kati ya jeshi la serikali na waasi wa RSF, Aprili mwaka 2023.
Watu 25 wauawa Nyala
Aidha, katika mji wa Nyala, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, mashambulizi ya anga ya jeshi la Sudan yaliwaua watu 25. Chanzo cha kitabibu ambacho hakikutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, kimeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa mashambulizi hayo yamefanyika kwa siku ya pili mfululizo katika mji wa Nyala, ambao ni eneo kubwa la kimkakati lenye uwanja mkubwa wa ndege kwenye jimbo la Darfur, liliko magharibi mwa Sudan, ambalo linashikiliwa na wanamgambo wa RSF, tangu mwishoni mwa 2023.
Kulingana na jeshi na picha za satelaiti zilizopatikana na Maabara ya Utafiti wa Kiutu ya Chuo Kikuu ya Yale, RSF inautumia uwanja huo wa ndege kusambaza na kusafirisha silaha zake.
Katika hatua nyingine, mtu mmoja aliyeshuhudia ameiambia AFP kuwa makombora ya RSF yaliushambulia mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, El-Fasher, mji pekee wa Darfur ambao hauko chini ya udhibiti wa wanamgambo. Katika jimbo la Kordofan Kusini lililopo umbali wa kilomita 700 kusini magharibi mwa Khartoum, zaidi ya watu 50 waliripotiwa kuuawa Jumatatu kwa makombora yaliyorushwa na kundi la Sudan People's Liberation Movement-North SPLM-N.
SPLM-N yalishutumu jeshi
Ofisi ya kiutu ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa mashambulizi hayo yalitokea kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Kadugli. Jana Jumanne, SPLM-N ililishutumu jeshi kwa kuyashambulia maeneo yake, ya Kordofan Kusini ambayo inayadhibiti, katika jaribio la kuyakomboa maeneo hayo.
Soma zaidi: Watu wa Sudan wanakabiliwa na hali ya kutisha
Wakati huo huo, watu waliyoyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano katika eneo la Wad Madani, wameanza kurejea makwao baada ya jeshi la Sudan kulikomboa eneo hilo kutoka mikononi mwa RSF. Mmoja wa raia wa Sudan wanaorejea, Tamador al-Sayed, amesema wameteseka vya kutosha, lakini Mwenyezi Mungu amesikia kilio chao.
''Tuna furaha sana kwamba tunarejea nyumbani ili kuungana tena na familia zetu, marafiki na majirani. Tuna matumaini tutafika salama,'' alisisitiza al-Sayed.
Mapigano nchini Sudan ambayo yamesababisha mauaji ya maelfu ya watu na wengine zaidi ya milioni 12 kuyakimbia makaazi yao, yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, wakati ambapo jeshi linapanga mashambulizi ya kuyadhibiti maeneo ya katikati mwa Sudan na mji mkuu, Khartoum.
(AFP)