1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marmoush mwiba kwa Holstein Kiel

30 Septemba 2024

Mshambuliaji wa Misri Omar Marmoush aliifungia timu yake ya Eintracht Frankfurt magoli mawili na kuilaza timu iliyopandishwa daraja Holstein Kiel magoli 4-2.

https://p.dw.com/p/4lFge
Bundesliga Holstein Kiel - Eintracht Frankfurt
Mshambuliaji wa Frankfurt Omar Marmoush baada ya kufunga dhidi ya Holstein KielPicha: Frank Molter/dpa/picture alliance

Hii ilikuwa ni katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani iliyochezwa Jumapili huko mjini Frankfurt.

Baada ya kufunga mawili, Marmoush alisaidia kuunda hayo mengine mawili na kwa ushindi huo sasa Frankfurt imepata ushindi wake wa nne mfululizo katika Bundesliga msimu huu. Mara ya mwisho Frankfurt kupoteza mechi ilikuwa ni mwanzoni mwa msimu ambapo walifungwa 2-0 na Bortussia Dortmund.

Marmoush hajawahi kufunga mabao katika mechi nne mfululizo za ligi kwenye taaluma yake ya kandanda katika klabu ya Frankurt. Hii inamaanisha kwamba Frankfurt kwa sasa wako pointi moja tu nyuma ya viongozi wa ligi Bayern Munich baada ya mzunguko wa tano wa mechi.

Bayern wabanwa na Leverkusen

Bayern walipoteza pointi zao za kwanza msimu huu baada ya kutoka sare ya bao moja na mabingwa Bayer Leverkusen hapo Jumamosi katika uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena.

Kocha wa Bayern Munich Vincent Kompany
Kocha wa Bayern Munich Vincent KompanyPicha: picture alliance/Peter Schatz

Kocha wa Bayern Vincent Kompany ana matumaini timu yake inaelekea kwenye mkondo unaostahili licha ya kupoteza pointi hizo muhimu dhidi ya hao watani wake.

"Ni mchezo mzuri tunaoupenda wa kandanda na wakati mwengine hata ukiwa na nafasi na ukatawala mchezo, huenda matokeo yasiende upande wako. Ila ilikuwa mechi nzuri. Kwangu mimi ilikuwa mechi ya hali ya juu, yenye shinikizo kubwa na nafikiri tumefanya tulichostahili kufanya katika mechi hii," alisema Kompany.

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso kwa upande wake amesema kwamba amefurahia jinsi walivyofanikiwa kujilinda vyema dhidi ya Bayern walioshambulia kwa jumla ya mashuti 18 katika mechi hiyo na hatimaye wakaishia kupata pointi muhimu.

Chanzo: Reuters/AP