Marekani yajitolea kuendeleza ushirikiano na nchi za Ghuba
8 Juni 2023Blinken alitoa kauli hiyo siku ya Jumatano wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri wa ushirikiano wa nchi za Ghuba kwa kifupi GCC, mjini Riyadh kufuatia mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan na kiongozi wa taifa hilo Mwanamfalme Mohammed bin Salman.
"Marekani ipo katika kanda hii na inaendelea kuwekeza katika ushirikiano na nyinyi nyote ili kujenga mustakabali imara na thabiti zaidi wa Mashariki ya Kati na kiukweli GCC ndio kiini cha maono yetu ya Mashariki ya kati iliyo imara, salama, yenye ufanisi na iliyounganika vyema," alisema Blinken.
Mikutano hiyo imefanyika siku moja baada ya Blinken kutua Jeddah, akianza ziaza inayolenga kuimarisha uhusiano na mshirika wake Saudi Arabia, ambayo imeanza kurejesha mahusiano ya karibu na mahasimu wa Marekani. Mahusiano ya miongo baina ya washirika hao wa zamani yaliingia dosari katika miaka ya hivi karibuni, haswa kutokana na masuala ya haki za binadamu na mafuta, baada ya wito wa Marekani wa kutaka bei za mafuta kupunguzwa mnamo mwaka jana kupuuzwa.
Ziara ya siku tatu ya Blinken ni ya kwanza tangu Saudia iliporejesha uhusiano wa kidiploamsia na Iran, ambayo imo katika mivutano na nchi za magharibi kufuatia shughuli zake za nyuklia na ushiriki wake kwenye mizozo ya kikanda. Siku ya Jumanne ambayo Blinken aliwasili, Iran ilifungua tena ubalozi wake mjini Riyadh baada ya kuufunga kwa miaka saba.
Siku hiyohiyo Mwanamfalme Salman alikuwa mwenyeji wa rais wa Venezuela Nicolas Maduro, mkuu wa nchi nyingine mzalishaji mkubwa wa mafuta ambaye kwa muda mrefu amekuwa kwenye mivutano na Washington.
Mkutano wa Jumatano wa GCCulihudhuriwa pia na waziri mkuu wa Qatar na kutawalaiwa na masuala muhimu ya kikanda ikiwa ni pamoja na mizozo ya Yemen, Sudan, Syria na mamlaka ya Palestina. Muda mfupi kabla ya mkutano huo, Blinken alifanya mazungumzo na mwanadiplomasia wa juu wa Saudia. Mawaziri hao wawili "walikubaliana kuendelea kufanya kazi pamoja kukabiliana na ugaidi, kuunga mkono juhudi za kuleta amani Yemen na kuimarisha utulivu na usalama, kupunguza mivutano na kuongeza ushirikiano wa kikanda".
Soma pia: Ziara ya Blinken Saudi Arabia, ina lengo gani?
Tangu kutangaza kurejesha uhusiano na Iran mwezi Machi, Saudi Arabia imerejesha uhusiano na mshirika wa Iran, Syria na kuongeza juhudi za upatikanaji amani nchini Yemen, ambako kwa miaka mingi imekuwa ikiongoza muungano wa kijeshi dhidi ya waasi wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran.