1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yahimiza utawala wakiraia baada ya Hamdok kujiuzulu

3 Januari 2022

Marekani imewahimiza viongozi wa Sudan kuzingatia utawala wa kiraia na kumaliza vurugu dhidi ya waandamanaji baada ya Abdalla Hamdok kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri mkuu.

https://p.dw.com/p/454oJ
Sudan Premierminister Abdalla Hamdok
Picha: AFP

Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alitangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo baada ya kushindwa  kuunda mkakati utakaokamilisha kipindi cha mpito. Hamdok ambaye kujiuzulu kwake kunaiweka Sudan katika njia panda kisiasa, amesema amejaribu kulizuwiya taifa kuingia katika maafa lakini ameshindwa kutokana na hali kuwa mbaya zaidi.

Mitandao ya kijamii nchini Sudan imekuwa na hisia mseto kufuatia kujiuzulu kwa Hamdok, baadhi ya watu wanasikitika kumpoteza kiongozi waliomtegemea kwa maarifa yake huku wengine wakiwa bado wamekasirishwa na kitendo cha Hamdok kurejea madarakani baada ya mapinduzi wakielezea juhudi zao kukatizwa za kusitisha utawala wa kijeshi.

Jibril Ibrahim, kiongozi wa zamani wa waasi aliyehudumu kama waziri wa fedha chini ya serikali ya Hamdok aliyeunga mkono jeshi kabla ya mapinduzi, ameitaja hatua ya Hamdok kama ya kujutia akisema Sudan inahitaji maelewano ya kisiasa wakati huu ili kuivusha salama katika nyakati hizi za misukosuko ya kisiasa.

Huku hayo yakiarifiwa kitengo kinachoshughulika na masuala ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani, kimesema baada ya Hamdok Kujiuzulu, viongozi wa Sudan wanapaswa kuweka kando tofauti zao kutafuta suluhu ya pamoja na kuhakikisha kuendelea kuwepo kwa utawala wa kiraia.

Sudan: Abdallah Hamdok aachia ngazi

Abdallah Hamdok ambaye ni mchumi na aliyewahi pia kushikilia nafasi katika shirika la Umoja wa Mataifa anayeheshimika sana katika jamii ya kimataifa, alihudumu kama waziri mkuu chini ya makubaliano ya kugawana madaraka kati ya jeshi na viongozi wa kiraia baada ya kiongozi wa muda mrefu nchini Sudan Omar al Bashir kuondolewa madarakani mwaka 2019.

Serikali ya kijeshi iliiondoa serikali ya Hamdok kupitia mapinduzi ya Oktoba 25 lakini akarejea mwezi mmoja baadae chini ya makubaliano yaliyompa nafasi ya kuunda serikali ya wasomi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2023.

Hamdok amekuwa mshirika muhimu kwa ulimwengu wa kimataifa wakati Sudan ikijaribu kujiimarisha baada ya kutengwa kwa miaka kadhaa na kuwekewa vikwazo chini ya kiongozi wa zamani Omar al Bashir. Sudan ilinuia kumaliza mgogoro wake wa kisiasa na hatimae kuungwa mkono na mataifa ya magharibi.

Chanzo: Reuters/afp