Marekani, Uturuki zakubaliana kumaliza tofauti Syria
16 Februari 2018Wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umetiwa doa na masuala kadhaa, Uturuki ilikasirishwa hasa na hatua ya Marekani kuliunga mkono kundi la wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria la YPG, ambalo inalichukulia kuwa la kigaidi.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari, na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani rex Tillerson amesema mataifa hayo mawili yana malengo sawa nchini Syria, na kuapa kuuchukulia kwa uzito, wasiwasi wa kiusalama wa Uturuki.
Katika pendekezo ambalo linaweza kuashiria hatua muhimu katika juhudi za kuondoa tofauti za washirika hao kuhusu Syria, afisa wa Uturuki alisema Uturuki imependekeza kwamba vikosi vya Uturuki na Markeani vinaweza kuwa pamona mjini Manbij.
Kuondolewa kwa YPG Manbij
Hatua kama hiyo inaweza kuchukuliwa ikiwa wapiganaji wa kundi la YPG wanajitoa kwanza na kwenda katika maeneo ya mashariki mwa Mto Euphrates, jambo ambalo Uturuki imekuwa ikilidai kwa muda mrefu.
"Tunataka kuratibu namna ya kutuliza maeneo kwa pamoja na nani atakalia maeneo hayo na malengo, nia ikiwa kurejesha vijiji hivi, miji hii kwa watu waliokuwepo kabla ya kutekwa na kundi la Daesh. Hivyo tutashughulikia kwanza Manbij. Ni mmoja ya maeneo tunayokwenda kuyafanyia kazi," alisema Tillerson.
Cavusoglu amesema Uturuki itaweza kuchukuwa hatua za pamoja na Marekani nchini Syria baada ya kundi la YPG kuondoka Manbij na maeneo ya jirani. Pia amesema mataifa hayo mawili yameanzisha mfumo kwa ajili ya mazungumzo zaidi, na watakutana tena kufikia katikati mwa mwezi Machi kuzungumza zaidi kwa lengo la kumaliza kabisaa tofauti zao.
"Laazima tuwe na uhakika wa hatua tutakazozichukuwa na laazima tuwe na uhakika kwamba YPG wanakwenda mashariki mwa Mto Euphrates. Laazima tuone utekelezaji. Ili maeneo haya yarejeshewe utulivu, suala la nani atayaongoza na kulinda usalama ni muhimu, na Rex Tillerson pia amelisema hili."
Mazungumzo hayo yalifuatia mkutano mrefu kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Cavusoglu na Tillerson Alhamisi usiku, ambapo masuala kadhaa ya mtafaruku yalijadiliwa.
Kiini cha mzozo kati ya Marekani na Uturuki
Pamoja na Syria, masuala hayo yalihusisha malalako ya Ankara dhidi ya kiongozi wa kidini wa Uturuki anaeishi uhamishoni nchini Marekani, ambaye Erdogana anamtuhumu kwa kupanga njama ya mapinduzi iliyoshindwa mwaka 2016, wasiwasi wa Marekani kuhusu demokrasia nchini Uturuki na upinzani dhidi ya mipango ya Uturuki kununua mifumo ya kinga dhidi ya makombora kutoka Urusi.
Uturuki inakasirishwa na inachokichukulia kuwa kusita kwa Marekani kumrejesha Fethullah Guleni, na kushtakiwa nchini Marekani, kwa mtendaji wa benki wa Kituruki anaetuhumiwa kuisaidia Iran kukwepa vikwazo.
Kwa upande wake Marekani inaghadhabishwa na kufungwa kwa waandishi wa habari na wapinzani, raia wa Marekani na wafanyakazi wa Kituruki kwenye balozi zake ndogo kwa madai ya kuhusika na ugaidi.
Ziara ya Tillerson imekuja wakati kukiwa na ongezeko la matamshi makali katika siku za karibuni dhidi ya Marekani kutoka kwa maafisa wa Uturuki, wakiwemo rais Erdogan na waziri Cavusoglu, huku rais Erdogan akisema wiki hii kuwa Wamrekani wanastahili kibao cha Ottoman, akimaanisha nguvu ya himaya ya Ottoman kwa wakati mmoja.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, Ape
Mhariri: Saumu Yusuf