1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Uturuki zatunishiana misuli

Sylvia Mwehozi
9 Oktoba 2017

Uturuki imeijibu Marekani kwa kuchukua hatua zinazofanana baada ya ubalozi wa Marekani mjini Ankara kutangaza jana Jumapili kwamba unasitisha mara moja huduma ya utoaji wa visa zisizo za wahamiaji. 

https://p.dw.com/p/2lUCW
Türkei Großkundgebung in Gaziantep mit Präsident Erdogan
Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Marekani imeeleza kwamba sababu ya kufanya hivyo ni kutathmini upya uwajibikaji wa serikali ya Uturuki katika usalama wa vituo vya Marekani na wafanyakazi wake. Katika taarifa yake iliyoitoa mjini Ankara, Marekani inasema "katika kupunguza idadi ya wageni katika balozi zetu wakati tathmini ikiendelea, tunasitisha mara moja huduma ya visa zisizo za wahamiaji katika vituo vyote vya kidiplomasia vya Marekani nchini Uturuki".

Masaa machache baadaye ubalozi wa Uturuki mjini Washington ulitoa kauli kama hiyo na kutoa orodha ya sababu kwa uamuzi wake pia wa kusitisha huduma ya utoaji wa visa zisizo za wahamiaji.

Uturuki imesema visa zilizositishwa ni pamoja na visa zinazotolewa katika pasipoti, visa za kielekroniki na zile zinazotolewa mpakani. Wiki iliyopita Marekani ilionyesha kusikitishwa na kukamatwa kwa mfanyakazi wake ambaye ni raia wa Uturuki katika ubalozi mdogo mjini Istanbul, ikikataa mashitaka dhidi yake.

G20 Gipfel in Hamburg | Erdogan & Trump
Rais Donald Trump alipokutana na Rais Tayyip Erdogan mjini Hamburg katika mkutano wa G20Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/Turkish Presidency

Balozi wa Marekani John Bass anayemaliza muda wake mjini Ankara amesema kukamatwa kwa mfanyakazi huyo kulichochewa zaidi na "kulipa kisasi badala ya haki".

Wamarekani kadhaa wanashikiliwa nchini Uturuki akiwemo mchungaji wa kikristo Andrew Brunson ambaye anaendesha kanisa dogo mjini Izmir magharibi mwa pwani ya Uturuki. Marekani inasema raia wake huyo amefungwa kimakosa wakitaka aachiliwe. Raia wa Ujerumani pia wanaoshikiliwa wamo waandishi wa habari wawili na mfanyakazi mmoja wa haki za binadamu, Peter Steudtner ambaye anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashitaka wa Uturuki.

Wanasiasa na wataalamu katika nchi zote mbili wameonyesha wasiwasi kwamba watu hawa wote ni "mateka". Vyombo vya habari vya Uturuki vina taarifa za kutosha kuhusu mfanyakazi aliyekamatwa. Ripoti zinasema alikamatwa kwa upelelezi na kudai kwamba ana mahusiano na wafuasi wa Fethullah Gulen ambaye anaishi nchini Marekani na aliye hasimu wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

Fethullah Gülen Türkei
Fethullah Gulen ambaye ni hasimu wa Rais ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/S.Suna

Hatua ya Marekani ya kusitisha huduma ya utoaji visa itawaathiri raia wa Uturuki ambao wana nia ya kuomba visa kwa kutumia vituo vya kidiplomasia nchini Uturuki. Aina ya visa zilizoathirika zaidi ni pamoja na zile za utalii, matibabu, biashara na kazi au masomo ya muda.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amezungumza na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uturuki. Ankara imekuwa ikiitaka Marekani kumrejesha Gulen inayemtuhumu kwa jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana.

Uturuki pia ina hasira na Ujerumani kwa kuwapatia hifadhi raia wa Uturuki wakiwemo wafuasi wa Gulen. Wakati huo huo Uturuki inazidi kuwa karibu na Urusi na Iran na kuleta wasiwasi kwa wanasiasa wa Marekani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/reuters

Mhariri: Josephat Charo