1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ukraine yaelekea Magharibi

27 Juni 2022

Hadhi ya uwanachama wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine na Moldova ndio hatua ya mwisho ya kuundwa upya bara hilo. Nyakati za maeneo ya kuzitenganisha Mashariki na Magharibi zinafikia kikomo, anasema Roman Goncharenko wa DW

https://p.dw.com/p/4DHlv
EU-Gipfel Kandidatenstatus für Ukraine und Moldau
Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya ni wa kihistoria – kwa jamhuri hizo za muungano wa zamani wa Soviet na pia kwa Umoja wa Ulaya. Ni mabadiliko muhimu. Ukraine imekuwa ikibisha kwenye mlango wa Umoja wa Ulaya kwa karibu miaka 20, lakini Brussels haikutaka kuufungua.

Soma pia:EU yazipa Ukraine na Moldova hadhi ya wagombea kujiunga

Ishara za kwanza zilitumwa katika miaka ya mwanzoni mwa milenia mpya na Rais wa kimabavu Leonid Kuchma, aliyetaka kudumisha usawa kati ya Urusi na nchi za Magharibi. Dirisha la fursa lilifunguliwa baada ya kuondoka kwake na ushindi wa kilichofahamika kama Vuguvugu la Chungwa mjini Kyiv mwaka wa 2004, wakati mwanasiasa aliyeegemea nchi za Magharibi Viktor Yushchenko alipomrithi. Lakini mambo hayakufanya kazi. Mabadiliko ya kidemokrasia nchini Ukraine yalifanyika sambamba na utanuzi wa kwanza muhimu wa Umoja wa Ulaya katika upande wa masharikii, ambao uliandamana na hofu miongoni mwa nchi za Magharibi mwa Ulaya ya kuwepo na utitiri wa vibarua vya malipo duni.

Wasiwasi huo haukutimia, lakini Umoja wa Ulaya ulisita kuendelea kujitanua kwa kasi hiyo hiyo. Kisha kukatokea mzozo wa kifedha mwaka wa 2009 na baadae mzozo wa uhamiaji wa 2015.

Roman Goncharenko
​​Roman Goncharenko wa DWPicha: DW

Ulaya Magharibi haikutaka Ukraine ijiunga na EU

Lakini sababu kubwa zaidi ya kwa nini Ukraine haijaweza kuruhusiwa kuwa karibu na Umoja wa Ulaya mpaka sasa ilikuwa ni upinzani wa wanachama waanzilishi wa Umoja wa Ulaya walio na ushawishi. Iliwafaa zaidi kwa sababu nchi hiyo kubwa iliweka aina fulani ya ukanda wa kuutenganisha Umoja wa Ulaya na Urusi. Ulaya Magharibi pia ilihofia kuwa uwanachama wa Ukraine ungebadilisha mizani kuelekea upande wa Mashariki na Ulaya ya Kati, ambayo Brussels tayari ilikuwa imeharibu uhusiano.

Soma pia:EU ipanue wigo wake kuelekea Moldova na Ukraine kujiunga 

Haikujadiliwa hadharani, lakini Ulaya Magharibi ilikubali kitambo kuwa Ukraine ingesaliwa kuwa ndani ya nyanja ya ushawishi wa Moscow, ukiyataja mahusiano ya muda mrefu kati ya kile kilichofahamika na maafisa wa Umoja wa Ulaya kama "nchi ndugu na watu wake.” Waukraine wenyewe walisisitiza hilo kwa kumchagua kiongozi aliyeungwa mkono na UrusiViktor Yanukovych kuwa rais, ambaye maneo yake ya kuiunga mkono Ulaya yalikuwa ya kuficha ukweli halisi.

Umoja wa Ulaya ulitumai kuwa Ukraine ingetidhishwa na Sera yake ya Ujirani na ukanda wa biashara huria. Hii ilikuwa hatari, kosa la kihistoria ambalo kwa njia isiyo ya moja kwa moja lilichangia kuanzisha vita vya sasa vya Urusi dhidi ya Ukraine: Ulaya haikutaka kuikaribisha Ukraine, wakati Urusi ilitaka kuivuta tena jamhuri hiyo ya zamani ya Soviet chini ya udhibiti wake – kwa gharama yoyote ile.

EU-Gipfel Kandidatenstatus für Ukraine und Moldau
Waukraine wanaonyesha shauku ya uhuru na demokrasia na wako tayari kuvilinda kwa hali na maliPicha: Nicolas Landemard/Zuampress/picture alliance

Azma iliyopuuzwa

Umoja wa Ulaya na Urusi zilipuuza azma ya Waukraine. Wakati waliandamana wakat iwa matukio mawili ya mapinduzi ya umma, mwaka wa 2004 na 2014, WaUkraine wanathamini uhuru na demokrasia kuliko kingine chochote. Na, pia wanaonyesha kila siku, kuwa wako tayari kufa katika kuvitetea. Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine sasa umeulazimu Umoja wa Ulaya kurekebisha kosa lake. Itasubiriwa kuona ni kiasi gani Brussels itaendeleza suala hilo. Bila shaka kutakuwa na majaribio ya kupunguza kasi ya mchakato huu, lakini mabadiliko ya mkondo hayawezekani tena, Hadhi ya uwanachama kwa Ukraine na nchi jirani Moldova ina maana kuwa enzi ya maeneo ya utenganisho katikati ya mwa UIaya yanafikia mwisho.

Nchi zilizokuwa sehemu ya Soviet zinaelekea Magharibi, muda unahesabika, Pazia jipya la Chuma linashushwa. Ni hatua ya mwisho ya mchakato wa kupangwa upya kwa bara ambao ulianza na kumalizika kwa Vita Baridi.

Mwishowe hakutakuwa na upendeleo

Na vipi kuhusu Georgia, ambayo mwaka wa 2013 ilikuwa nchi ya kwanza ya uliokuwa muungano wa Soviet kutangaza kuegemea Magharibi kupitia kilichofahamika kama "Vuguvugu la Waridi?” Serikali mjini Tbilisi iliwasilisha ombi la uwanachama kwa Umoja wa Ulaya kwa wakati mmoja na Kyiv na Chisinau, lakini haikupata ridhaa.

Umoja wa Ulaya ulisema tu Georgia ina ilichokiita kuwa mtizamo wa Ulaya. Sababu kadhaa zilitolewa – ikiwemo mzozo wa kisiasa wa 2020, ambapo baada ya uchaguzi wa bungee upinzani uliituhumu serikali kwa undanganyifu katika uchaguzi. Brussels imefanya uamuzi sahihi kwa kuelewa bayana kwa Tbilisi kuwa haitayafumbia macho matatizo kama hayo. Hata kama kumekuwepo na mafanikio makubwa. Uamuzi kuhusu Georgia pia ni ishara kwa Ukraine na Moldova kutotarajia upendeleo mwishowe. Nchi hizo zitapaswa kuthibitisha kwa vitendo kuwa ziko tayari kwa utangamano zaidi na mageuzi yenye uchungu. Lakini hapana shaka: Zitafaulu na kujiunga na Umoja wa Ulaya. Na haraka kuliko wengi wanavyodhani.

Mwandishi: Roman Goncharenko 
Tafrisi: Bruce Amani