1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa mazungumzo nchini Burundi

13 Novemba 2015

Kwa miezi sasa watu wanauliwa nchini Burundi. Hakuna anaeshitakiwa. Kwa mara nyengine tena Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linaingilia kati hata kama azimio lililopitishwa si kali hivyo

https://p.dw.com/p/1H5Ka
Dirke Köpp mkuu wa matangazo ya kifaransa ya DWPicha: DW

Si makubwa yaliyofikiwa kama ufumbuzi na baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu Burundi alkhamisi iliyopita.Wanataka visa vya umwagaji damu vikome mara moja na yaanzishwe mazungumzo-la sivyo watawekewa vikwazo.Mazungumzo-serikali ya rais Pierre Nkurunziza haiko tayari.Na vikwazo vinavyotishiwa kuwekwa-si chochote chengine isipokuwa chui asiyekuwa na meno.Ni sawa na vikwazo vya Umoja wa ulaya vilivyoanza zamani kufanya kazi,lakini havijaleta tija yoyote hadi sasa.Kipi anaweza kukitekeleza mjumbe aliyeteuliwa hivi sasa na Umoja wa Mataifa,na hilo pia, jibu lake hakuna alijuaye.Kwa sabababu hata baada ya uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,hakuna si wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wala si wanajeshi wa kuingilia kati wa Umoja wa Afrika waliopelekwa Burundi ili kuzuwia mauwaji.Hilo baraza la usalama limeshindwa kulitamka .

Hali nchini Burundi imeharibika tangu mwishoni mwa mwezi wa April.Wakati ule watu waliteremka majiani kulalamika dhidi ya mhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.Jibu lake:matumizi ya nguvu.Miezi sita iliyopita ikafanyika njama ya kumpinduwa.Njama hiyo ikashindwa na matokeo yake yakawa matumizi zaidi ya nguvu.Juhudi zote zilizofanywa nje na ndani zilikuwa za bure,Pierre Nkurunziza akachaguliwa tena katika zoezi lililozusha mabishano na kuiongoza nchi hiyo tangu wakati huo kwa msaada wa wanamgambo wanaobeba silaha,ukandamizaji na mauwaji.

Kitisho cha mauwaji ya halaiki kimezagaa Burundi

Haipiti siku ambapo maiti hazionekani majiani katika mji mkuu Bujumbura na kwengineko nchini humo.Zaidi ya watu 250,kwa mujibu wa duru huru,wameuliwa tangu mwezi Aprili mwaka huu nchini Burundi.Makosa waliyoyafanya-kutoelemea upande wa serikali.Pekee mwezi uliopita Umoja wa Mataifa umeorodhesha visa 400 vya watu waliokamatwa,40 walioteswa na idara ya upelelezi ya Burundi.Watu wangapi wanatishwa,hakuna ajuaye.Vyombo huru vya habari hakuna tangu njama ya mapinduzi iliposhindwa.Vituo vya kibinafsi vya matangazo ya Radio vimevunjwa-waandishi habari wasiopungua 100 wamekimbilia nchi za nje.

Mkakati wa wafuasi wa Nkurunziza hadi wakati huu ulikuwa kuonyesha kana kwamba hali nchini humo ni shwari isipokuwa makundi madogo madogo tu ya wafanya fujo.Mnamo siku na wiki zilizopita matamshi yanayotolewa ni ya kutisha:wanazungumzia kuhusu "kazi",na "harakati" na kwamba "hakuna hisia wala huruma."Kazi,neno hilo kwa mjerumani halimaanishi kitu.Lakini kwa watu nchini Burundi au Rwanda neno hilo linakumbusha kumbukumbu mbaya kabisa za mauwaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda miaka 21 iliyopita.Wakati ule neno "Kazi" au "fanyeni kazi" lilikuwa likitumiwa kumaanisha "kuuwa."Wahanga walikuwa watu wa jamii ya wachache-Tutsi lakini pia wahutu wa msimamo wa wastani.Zaidi ya watu 800 000 waliuliwa nchini Rwanda wakati ule.Kila mahala ulimwenguni watu walipaza sauti wakisema "kamwe yasitokee".Ukaibuka mkakati unaoubebesha Umoja wa Mataifa jukumu la kinga.

Hali nchini Burundi inafanana na ile ya Rwanda ya mwaka 1994.Na matamshi yanayotolewa mnamo wiki za hivi karibuni yamezidi kuwagutua walimwengu.Na sasa hatimae Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetamka-kwa kupitisha angalao hicho kiazimio kidogo.Uamuzi mzito ni kitu chengine kabisa.Hata hivyo hii ni hatua ya mwanzo kumuonesha rais wa Burundi na kundi lake kwamba wanachunguzwa.

Mwandishi:Köpp,Dirke/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Gakuba Daniel