Maoni: Kushindwa kwa Marco Rubio
17 Machi 2016Uwezekano kwamba chama cha Republican kitaamua kumteua mgombea wake kuwania urais wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu umeongezeka tangu siku ya Jumanne Kabambe, licha ya bilionea Donald Trump kuendelea kushinda katika chaguzi za mchujo na Marco Rubio akijiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwania uteuzi wa chama hicho.
Marco Rubio alifanya kila aliloweza lakini juhudi zake hazikutosha. Seneta huyo alishindwa katika uchaguzi wa mchujo katika jimbo lake la Florida. Kwa mara nyingine tena bilionea Donald Trump aliibuka na ushindi. Kipigo kikubwa cha aibu kwa Rubio. Rubio halazimiki tu kuachana na azma yake ya kuwa rais wa Marekani, bali pia huenda pengine ikawa ndio mwisho wake kisiasa, angalau kwa miaka miwili au mitatu ijayo.
Kwa nini Rubio alishindwa?
Kwanza kabisa, anatakiwa ajilaumu mwenyewe. Rubio aliona Trump anagonga vichwa vya habari kwa kuwatusi mahasimu wake kisiasa. Seneta huyo mwenye umri wa miaka 44 lazima alidhani: "Naweza kufanya hivyo pia mimi". Alianza kujiingiza katika siasa chafu za malumbano. Rubio aligeuka kuwa mpinzani wa Trump na msimamo huu ungeshindwa tu. Kwa wapiga kura Trump anawavutia sana kuliko Rubio.
Lilikuwa kosa kwa Rubio kujivunjia heshima na kuishusha hadhi yake kufikia kiwango cha Trump. Rubio alipoteza muda akihoji kuhusu uwezo wa Trump badala ya kuelekeza nguvu katika kuwaeleza wapiga kura kuhusu uwezo wake, kama vile uzoefu wake katika masuala ya nchi za kigeni na sera ya ulinzi au mawazo kuhusu jinsi sera ya uhamiaji inavyoweza kufanya kazi.
Mashambulizi ya Rubio dhidi ya Trump yalionekana kama kitendo cha kukata tamaa. "Hivyo sivyo rais mtarajiwa anavyotakiwa kuonekana," ndivyo walivyohisi wapigaji kura wengi. Waliacha kumuunga mkono.
Rubio hakuwa na ujumbe wowote wa kuvutia na uliokubalika na Wamarekani. Katika hotuba zake alizungumzia ndoto yake ya uchumi wa karne ya 21. Lakini wengi walijiuliza alikuwa na maana gani hasa. Kwa kulinganisha, ahadi za Trump kujenga ukuta kuwazuia wahamiaji wasiingie Marekani, kuweka vikwazo vya kiuchumi kulilinda soko la Marekani, ziko wazi kabisa na zinaeleweka. Ukweli kwamba sio lazima ahadi hizo zifaulu kuyatatua matatizo, ni suala lengine.
Rubio pia alishindwa kwa sababu ya pesa. Wadhamini wa chama cha Republican walichelewa kuiunga mkono kampeni yake. Viongozi wa chama hicho walianza kumsaidia baada ya Jeb Bush kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Bush hakumsamehe Rubio kwa kushindana naye kutaka kura za wapiga kura sawa, na pia kwa kutaka kuingia ikulu. Licha ya maombi kadhaa, familia ya Bush, ambayo ina ushawishi fulani katika jimbo la Florida, ilikataa kumuunga mkono katika siku chache zilizopita. Ulimwengu wa siasa unaweza kuwa na ukatili, hususan nchini Marekani.
Kushindwa kwa Rubio kutakuwa na athari. Trump amesonga hatua moja karibu na kushinda uteuzi wa chama cha Republican kuwa mgombea urais. Uongozi wa chama uko taabani, una wasiwasi. Warepublican wenye misimamo ya wastani sasa wanaweka matumaini yao kwa gavana wa jimbo la Ohio, John Kasich, lakini Trump tayari anaelekea kupata ushindi.
Clinton atamba kambi ya Democratic
Kwa upande wa chama cha Democratic, mchuano si wa kusisimua sana. Hillary Clinton anabaki kuwa mgombea anayependelewa, lakini seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders, hatarajiwi kukubali kushindwa kirahisi hivyo. Lengo lake sio tena kuwa rais. Anataka kumlazimisha mpinzani wake ayazingatie masuala ambayo yamekuwa moyoni mwake.
Sanders anataka sheria kali zaidi za kusimamia Wall Street na fedha zaidi kwa ajili ya elimu na miundo mbinu, anataka mikataba ya biashara huru kati ya nchi 12 za eneo la Pacific TTP na mkataba wa kibiasahra kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya, TTIP, ifutiliwe mbali. Clinton atalazimika kuyakubali baadhi ya malengo. Vinginevyo, Sanders na wafuasiw ake huenda wakakataa kumuung amkono na hivyo Trump huenda akawa rais wa Marekani. Mungu aepushe mbali.
Mwandishi:Soric,Miodrag
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri:Yusuf Saumu