1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hakuna sababu ya 'Obamamania' Afrika

28 Julai 2015

Rais Obama amekamilisha ziara yake Kenya na Ethiopia. Alikuwa na maneno matamu ya kuzikonga nyoyo za watu. Lakini ziara yake haitaleta mageuzi chanya anasema Daniel Pelz wa DW.

https://p.dw.com/p/1G6Yd
Äthiopien Addis Abeba Obama Rede Afrikanische Union
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Ziara ya Barack Obama Afrika Mashariki ilikuwa ziara ambayo ingemfanya mhadhiri yeyote wa sera za kigeni kuwa na fahari. Obama alifika, akaona na akasema kitu kilichostahili kila mahala alipokuwa: Miito ya heshima kutaka haki za binaadamu na demokrasia viheshimiwe kuyaridhisha makundi ya kijamii, kauli za kutia moyo kwamba Afrika inaweza kuyatatua matatizo yake yenyewe na kwamba alikuwa na ari inayohitajika kuimarisha ushirikiano na Kenya na Ethiopia katika masuala ya usalama na biashara.

Lakini Mkuu wa Idhaa ya Kiingereza ya DW Afrika Link Daniel Pelz anasema huku ndege ya Air Force One ikiwa angani kwenda Washington na barabara za Nairobi zikirejea katika maisha ya kawaida, jambo moja liko wazi kabisa: Hakuna sababu ya kuwa na jazba kuhusu Obama - Obamamania - barani Afrika na hakukuwa na sababu yoyote hapo kabla. Bingwa huyo wa demokrasia na haki za binaadamu mwenye maono makubwa aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2009 imeondoka jukwaani. Ukweli ni kuwa hali ya kisiasa imechukua mahala pake. Ulimwengu hautakuwa mahala pazuri zaidi pa kuishi wakati Obama atakapoondoka ikulu mwaka 2016 na vile vile bara la Afrika hali itakuwa hiyo hiyo.

Biashara kama kawaida haileti mageuzi

Miito yake kuwataka Wakenya kujiepusha na siasa za kikabila na kuukabili ufisadi haitasaidia kitu. Wakenya waliacha kuhesabu mara nyingi waliposikia miito ya aina hiyo kutoka kwa viongozi mashuhuri wa kigeni na mara ngapi waliposikia ahadi kutoka kwa wanasiasa wao kukomesha kabisa ukabilia na rushwa. Ama kweli Wakenya hawahitaji kusikia miito ya aina hii kwa sababu wengi wao wana ndoto iliyo wazi ya nchi wanamotaka kuishi. Wanachokosa ni wanasiasa wanaohitajika kuitekeleza miito hii kwa vitendo na kuwa ukweli. Ziara za hapa na pale na hotuba za kusisimua hazitaifanya Kenya kuwa nchi nzuri zaidi.

Kama Obama angetaka kweli kuleta mabadiliko katika taifa ambalo babake alizaliwa, hangekutana na kuzungumza na rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Willaim Ruto. Mahakama ya kimaitaifa ya uhalifu, ICC iliwashitaki viongozi hao wawili kwa kuwa miongoni mwa watu waliopanga machafuko ya kikabila baada ya uchaguzi wa mwaka 2008.

Pelz Daniel Kommentarbild App
Mkuu wa Afrika Link, Daniel Pelz

Kuitisha mageuzi lakini wakati huo huo kuendelea na shughuli kama kawaida katika masuala ya usalama na biashara haipeleki kokote. Kuvisaidia vikosi vys usalama vya Kenya, vinavyojulikana kwa rushwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, haiifanyi miito yake kuwa ya kuaminika.

Maneno matamu kuibusu demokrasia na haki za binaadamu

Kama Kenya ilikuwa haitoshi kuonyesha pengo lililopo kati ya maono ya Obama na sera ya sasa ya Marekani kuelekea Afrika, basi ziara yake nchini Ethiopia inatosha. Obama aliitembelea nchi ambayo chama cha waziri mkuu Hailemariam Desalgn kinalidhibiti bunge. Nchi ambayo uhuru wa vyombo vya habari unakabiliwa na kitisho kikubwa na viongozi wa upinzani wanatishwa na vikosi vya usalama.

Obama aliitisha nafasi pana zaidi ya demokrasia kwa Waethiopia wote, heshima zaidi kwa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binaadamu ziheshimiwe zaidi. Kisha akakubali kurefusha ushirikiano na vikosi vya usalama vya Ethiopia katika vita dhidi ya kundi la wanamgambo wa kiislamu la al Shabaab katika nchi jirani ya Somalia.

Hizo ni habari njema kwa serikali ya Ethiopia. Ni kitu sahihi cha kufanya kwa rais wa Marekani anayetaka kuilinda nchi yake kutokana na kitisho cha al Shabaab. Lakini je, ni ujumbe gani anaoutoa kwa upinzani wa Ethiopia na makundi ya kijamii yanayohisi yanakabwa koo na vikosi hivi vya usalama kila uchao?

Katika hotuba yake ya kusisimua mbele ya Umoja wa Afrika, Obama alionyesha taswira yake ya mtu mwenye maono ndani yake. Waliomsikiliza walimsikiliza kwa umakini mkubwa alipowapa changamoto viongozi wa Afrika wauheshimu muda wa mihula ya uongozi na waondoke madarakani. Jinsi aliposisitiza anavyoyatarajia maisha nje ya ikulu. Alipowasihi wajumbe waiangamize rushwa mara moja.

Lakini kuibadili Afrika ni suala linalohusu zaidi vitendo badala ya maneno. Ikiwa Obama anataka kweli kuleta mabadiliko barani Afrika alikotokea babake, anatakiwa ayageuze maono yake kuwa sera ya serikali yake. Vitendo vyake vya sasa havitaifanya Afrika kuwa mahala pazuri zaidi.

Mwandishi:Daniel Pelz

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Daniel Gakuba