1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yampa balozi wa Ufaransa saa 72 kuondoka nchini humo

31 Januari 2022

Mali imemfukuza balozi wa Ufaransa kuhusiana na "matamshi ya kiuadui" yaliotolewa na maafisa wa mkoloni wake wa zamani, katika ongezeko jipya la mzozo kufuatia mapinduzi ya kijeshi. Uhusiana wa mataifa hayo umedorora.

https://p.dw.com/p/46KK1
Mali | Übergangspräsident Assimi Goïta
Picha: Präsidentschaft der Republik Mali

"Serikali ya Jamhuri ya Mali inaufahamisha umma wa kitaifa na kimataifa kwamba leo...balozi wa Ufaransa mjini Bamako, Mh. Joel Meyer..aliarifiwa juu ya uamuzi wa serikali kumuomba aondoke katika ardhi ya taifa katika muda wa masaa 72," ilisema taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa.

Uhusiano kati ya Mali na Ufaransa umezorota tangu jeshi lilipotwaa madaraka mnamo Agosti 2020.

Wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliwaambia waandishi habari kwamba utawala wa kijeshi wa Mali ulikuwa "haramu" na maamuzi yake "siyo ya uwajibikaji."

Soma pia: Viongozi wa Mali wajiuzulu kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Waziri wa ulinzi Florence Parly aliwatuhumu watawala wa taifa hilo la Afrika Magharibi kwa kuongeza kila alichokiita "uchokozi" dhidi ya Ufaransa.

UN I Jean-Yves Le Drian
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian.Picha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Taarifa ya Jumatatu imesema matamshi yametolewa ambayo ni ya "kiuadui na ya kuchukiza," na yalitolewa licha ya upinzani wa mara kwa mara kutoka Mali.

"Serikali ya Mali inalaani vikali na inakataa matamshi hayo, ambayo yanakwenda kinyume na uhusiano wa kimaendeleo na kirafiki kati ya mataifa hayo," ilisema.

Undumila kuwili kuhusu mapinduzi

Hata hivyo, iliongeza kuwa, serikali ya Mali inakariri utayarifu wake kuendeleza majadiliano na kutafuta ushirikiano na washirika wake wote wa kimataifa, ikiwemo Ufaransa, kwa njia ya kuheshimiana na kwa msingi wa kanuni kuu ya kutoingiliana."

Wanajeshi waongoza mapinduzi Mali

Soma pia:Mali yatangaza serikali mpya yenye maafisa wa kijeshi

Waziri wa mambo ya nje wa Mali Abdoulaye Diop aliituhumu Ufaransa siku ya Ijumaa kwa kuonyesha ghadhabu za kuchagua linapokuja suala la utawala wa kijshi.

"Ufaransa, ambayo inasema inatetea demokrasia, imekwenda katika mataifa mengine na kuwaweka wakuu wa serikali waliofanya mapinduzi, imewasifu," alisema.

Ufaransa ina maelfu ya wanajeshi waliopelekwa kanda ya Sahel kuisaidia Mali, pamoja na Niger na Burkina Faso, zinazokabiliwa na uasi mbaya wa makundi ya wapiganaji wa itikadi kali.

Mali Frankreich Truppen verlassen Timbuktu
Baadhi ya wanajeshi wa Ufaransa waliko nchini Mali.Picha: Blondet Eliot/ABACA/picture alliance

Mzozo umeongezeka tangu jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, ilipotangaza vikwazo vya kibiashara na kufunga mipaka na Mali mapema Januari, katika hatua iliyoungwa mkono na Ufaransa, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Soma pia: Mwanaume aliejaribu kumuuwa rais wa Mali afariki jela

Vikwazo hivyo vilifuatia pendekezo la utawala wa kijeshi kusalia madarakani kwa hadi miaka mitano kabla ya kuandaa uchaguzi, licha ya hapo awali kuahidi kuitisha uchaguzi kufikia mwishoni mwa Februari 2022.

Maafisa waasi waliongoza mapinduzi mnamo Agosti 2020 yaliomuondoa rais wa Mali aliechaguliwa kidemokrasia Ibrahim Boubacar Keita, aliekuwa akikabiliwa na maandamano ya hasira kuhusiana na kushindwa kwake kuwadhibiti wapiganaji wa Kiislamu.

Chanzo: afpe.