1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Makombora kadhaa ya Urusi yarushwa Ukraine

26 Januari 2023

Ukraine imetangaza tahadhari ya uvamizi wa anga kwa nchi nzima mapema leo Alhamisi, huku maafisa wa usalama wakisema vitengo vya ulinzi wa angani vimekuwa vikijibu mashambulizi ya makombora kutoka Urusi.

https://p.dw.com/p/4Mjsl
Makombora ya Urusi yarushwa Ukraine siku moja baada nchi za magharibi kukubali kuipa Kyiv vifaru
Makombora ya Urusi yarushwa Ukraine siku moja baada nchi za magharibi kukubali kuipa Kyiv vifaruPicha: Daniel Cole/AP/dpa/picture alliance

Uvamizi huo unatokea baada ya Marekani na Ujerumani kuidhinisha mipango ya kuipa Ukraine vifaru vya kivita ili kuisaidia kupambana na mashambulizi dhidi ya Urusi, ambayo imekosoa vikali hatua hiyo na kuitaja kuwa hatari.

Jeshi la Ukraine limesema usiku wa kuamkia leo kwamba, kwa kutumia mifumo ya kujilinda na makombora limefanikiwa kuziharibu ndege 24 zisizokuwa na rubani kutoka Urusi, ikiwemo 15 zilizoangushwa karibu na mji wa Kiev. Hadi sasa hakuna ripoti za uharibifu wowote kufuatia tukio hilo huku maafisa wa usalama wakiwataka raia kuendelea kujilinda.

Urusi imekuwa ikilenga miundo mbinu muhimu katika mashambulizi yake Ukraine, kwa kutumia makombora na ndege hizo zisizokuwa na rubani kuanzia mwezi Oktoba  na kusababisha maeneo mengi kuwepo bila umeme katika kipindi hiki cha majira ya baridi.

Ujerumani yatuma vifaru kwa Ukraine

Kansela wa Ujerumani ametangaza kupelekwa kwa vifaru vya chapa Leopard 2 kwa Ukraine
Kansela wa Ujerumani ametangaza kupelekwa kwa vifaru vya chapa Leopard 2 kwa UkrainePicha: Philipp Schulze/dpa/picture alliance

Mapema hapo jana rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy aliisifia hatua ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na mwenzake wa Marekani Joe Biden kujitolea kuipa nchi yake vifaru vya kivita aina ya Leopard 2 na M1 Abrams huku akiwatolea mwito washirika wa Ukraine kutuma zana hizo za kijeshi haraka iwezekanavyo.

Ukraine imekuwa ikipambana kupata silaha zaidi ili kulipiga jeki jeshi lake latika mapambano yake na wanajeshi wa Urusi kwa nia ya kuyadhibiti pia maeneo yaliotwaliwa upande wa kusini na Mashariki tangu taifa hilo lilipoivamia tarehe 24 Februari mwaka 2022.

Hata hivyo Urusi kupitia balozi wa Urusi nchini Ujerumani Sergei Nechayev imesema hatua ya Ukraine kupema silaha zaidi ni hatari na huenda ukatanua mgogoro uliopo katika kiwango kipya.

Mapigano makali Bakhmut

Lakini rais Joe Biden amesema zana za kijeshi zilizotolewa kwa Ukraine hazitoi hatari ya aina yoyote kwa Urusi. Biden amesema silaha hizo zinahitajika kuisaidia Ukraine kuimarisha uwezo wao wa kujikinga katika uwanja mpana wa mapambano.

Huku hayo yakiarifiwa mapigano makali yameripotiwa katika eneo la Bakhmut. Wanajeshi huko wanasema Urusi inawashambulia kutoka ardhini kwa lengo la kudhibiti eneo zima la Donetsk.