Makampuni mawili ya majani ya chai ya Kenya yafutiwa vibali
12 Mei 2023Rain Forest Alliance ambalo ni moja ya mashirika makubwa ya kuidhinisha bidhaa za maendeleo endelevu duniani, limesema lilianzisha uchunguzi baada ya makala moja ya shirika la utangazaji la Uingereza BBC mwezi Februari kuangazia madai ya kusambaa kwa matukio ya unyanyasaji wa kingono katika mashamba ya majani ya chai. Uamuzi wa shirika hilo unamaanisha sasa Kampuni ya James Finlay (Kenya) Ltd na ile ya ekaterra Tea Kenya Plc, haziwezi tena kuuza bidhaa zao kupitia kibali cha shirika hilo. Kenya ni moja ya wasafirishaji wakubwa wa bidhaa hiyo. Kampuni ya Rainforest Alliance imesema bado inaendelea kuahidi kutimiza wajibu wake kusaidia kukomesha unyanyasaji wa kingono pamoja na ukatili wa majumbani katika mtandao wa kusafirisha majani chai duniani.