1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Syria yadhibiti kaskazini mwa Aleppo

Caro Robi
28 Novemba 2016

Shirika la kutetea haki za binadamu Syria limesema leo waasi wa Syria wamelipoteza eneo lote la kaskazini mwa mji wa Aleppo katika operesheni inayofanywa na jeshi kuudhibiti kikamilifu mji huo.

https://p.dw.com/p/2TLgJ
Syrien syrische Soldaten in Darayya
Picha: picture-alliance/Photoshot/Y. Zhen

Majeshi ya serikali ya Syria yanadhibiti thuluthi moja ya mji unaodhibitiwa na waasi wa Aleppo, baada ya mapambano makali mwishoni mwa wiki yaliyosababisha takriban raia 10,000 kuutoroka mji huo.

Katika mojawapo ya mafanikio yake makubwa katika azma ya kuudhibiti kikamilifu mji wa Aleppo, majeshi yaliyakomboa maeneo sita ya mashariki mwa mji huo mwishoni mwa wiki, likiwemo eneo la Masaken Hanano ambalo ndilo kubwa mashariki mwa mji huo.

Hapo jana, siku ya 13 ya operesheni, majeshi pia yaliyadhibiti maeneo ya Jabal Badra na Baadeen na kuyachukua maeneo mengine matatu. Shirika la kutetea haki za binadamu Syria limesema majeshi yanadhibiti pia maeneo mengi ya kaskazini mwa mji huo wa pili kwa ukubwa Syria.

Maelfu ya raia wautoroka mji wa Aleppo

Mkurugenzi wa shirika hilo la kutetea haki za bindamu Rami Abdel Rahman amesema waasi wamepoteza asilimia 30 ya maeneo ambayo walikuwa wanayadhibiti mjini humo na kuongeza kiasi cha raia 10,000 wameutoroka mji huo tangu siku ya Jumamosi, 6,000 kati yao wakitorokea mji wa kikurdi wa Sheikh Maksoud na wengine katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Syrien Flüchtlinge Aleppo
Raia wakiutorka mji wa AleppoPicha: Reuters

Abdel Rahman amesema hii ndiyo mara ya kwanza kushuhudia idadi kubwa ya raia wakiondoka Aleppo tangu mwaka 2012. Takriban raia 250,000 waliozingirwa kwa miezi kadhaa mjini humo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi.

Yasser al Youssef wa kundi la waasi la Nureddin al Zinki amesema wapiganaji wanajaribu kujikusanya katika eneo la Sakhur ili kuulinda mji huo na wakaazi wake lakini mashambulizi makali ya angani yanaharibu karibu kila kitu mjini humo.

Kudhibitiwa kwa  eneo la  Sakhur, liloko mashariki mwa Aleppo, inamaanisha mji huo Aleppo utagawanyika mara mbili kaskazini na kusini na kuwa pigo kubwa kwa upinzani. Kiasi cha raia 225 wakiwemo watoto 27 wameuawa katika mapambano hayo tangu tarahe 15 mwezi huu.

Majeshi yapania kuudhibiti mji kikamilifu

Umoja wa Mataifa una mipango ya kufikisha misaada, kuwoandoa walio wagonjwa na waliojeruhiwa. Waasi wameukubali mpango huo lakini serikali bado haijaridhia. Hakikisho pia linahitajika kutoka kwa Urusi-mshirika wa utawala wa Syria.

Syrien Aleppo Kampfhandlungen in zerstörter Stadt
Majeshi ya Syria Picha: picture-alliance/dpa

Wachambuzi wanasema utawala wa Rais Bashar al Assad unapania kuudhibiti mji huo wakati huu ambapo sera za kigeni za Marekani zinatarajiwa kubadilika.

Wakati huo huo, Misri imekanusha taarifa zilizotangazwa katika vyombo vya habari vya nchi kadhaa za kiarabu kuwa zimetuma majeshi yake nchini Syria, siku chache baada ya Rais Abdel Fattah al Sisi kutangaza analiunga mkono jeshi la Syria.

Wizara ya mambo ya nje ya Misri imesema madai hayo yapo katika fikra za wanaozikuza taarifa hizo. Mzozo huo wa Syria ambao umedumu kwa miaka sita sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu na mamilioni ya wengine kuachwa bila ya makazi.

 

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo