1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi Pakistan wasema uvumilivu wao umejaribiwa kwa muda

2 Novemba 2018

Kuachiliwa kwa mwanamke mmoja muumini wa Kikristo nchini Pakistan ambaye alisamehewa na mahakama miaka minane baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa kukufuru, kumecheleweshwa leo.

https://p.dw.com/p/37YQg
Pakistan, Lahore: Todesurteil gegen Christin in Pakistan aufgehoben
Picha: picture-alliance/dpa/K.M. Chaudary

Wakili anayemwakilisha mhubiri mmoja wa dini ya Kiislamu ambaye aliwasilisha mashtaka ya kukufuru dhidi ya mwanamke huyo Asia Bibi, jana Novemba Mosi, aliitaka Mahakama ya Juu zaidi kubadili uamuzi wake wa kumuondolea mashtaka Bibi. Mahakama ilibatilisha uamuzi wa mwaka 2010 uliomhukumu Bibi kifungo cha maisha kwa kosa la kumkejeli mtume Mohammad.

Tangu uamuzi huo kutolewa Waislamu wamekuwa wakifunga barabara kuu na kuharibu au kuteketeza magari ili kuishinikiza serikali kuzuia mwanamke huyo asiachiliwe. Waumini hao walitarajiwa kuandamana baada ya suala ya Ijumaa, jambo ambalo limezua hofu ya kutokea ghasia. Shule na vyuo zimefungwa nchini Pakistan baada ya mhubiri Kadim Hussain Rizvi, ambaye ni kiongozi wa chama cha Tehreek-e-Labbaik kutangaza kuwa mazungumzo kati yao na serikali yameshindikana.

Pakistan Proteste nach Freispruch Asia Bibi
Wafuasi wa chama cha Tehreek-e-Labbaik wafunga barabara na kuteketeza magari kupinga uamuzi wa mahakama kumsamehe Asia BibiPicha: Getty Images/AFP/R. Tabassum

Mmoja wa wakazi Najam Khan amesema,"Mji wote unaishi kwa hofu. Kutokana na hofu,hakuna anayetoka nje, kwasababu ya hali ya kukosekana utulivu. Barabara nyingi ziko kimya, hakuna usafiri. Watu wanatembea kwa miguu. Wale wanaomiliki magari ndio wenye nafuu, lakini hakuna usafiri wa umma.´´

Huduma za simu katika miji mikuu nchini Pakistan zimekatizwa huku vyama vya kidini vikijiandaa kuandamana dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi. Maandamano hayo yanajiri baada ya Waziri Mkuu Imran Khan kukikosoa  chama  cha Tehreek-e-Labbaik na kusema serikali haitavumilia maandamano ya ghasia.

Islamabad Ausschreitungen wegen Gerichtsurteil Blasphemie Straßensperre Container
Maafisa wa usalama waweka makontena barabarani kuwazuia waandamanji karibu na makutano ya mji wa Faizabad,Picha: Reuters/F. Mahmood

Maafisa wa usalama wameimarisha doria karibu na kituo anakozuiliwa bibi kuhakikisha usalama wake. Jana Alhamisi maafisa wa gereza walisema kuwa wanaume wawili walikamatwa mwezi uliopita kwa kupanga kumuua Bibi kwa kumnyonga. Wanaume hao bado wanahojiwa. Familia ya Bibi ilitarajia kuwa angeachiliwa jana. Licha ya kuwa familia yake haijafichua nchi atakayoishi baada ya kuachiliwa, lakini Ufaransa na Uhispania zimejitolea kumpa hifadhi.

Hayo yakijiri majeshi ya Pakistan yameonya leo kuwa uvumilivu wake umewekwa kwenye majaribu kwa muda baada ya kupewa vitisho na waislamu wenye itikadi kali. Msemaji wa jeshi  Asif Ghafoor amesema wanavumilia matamshi yanayotolewa dhidi yao lakini hatua inaweza kuchukuliwa kulingana na sheria na Katiba.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/APE

Mhariri: Saumu Yusuf