1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Maisha ya Papa Mstaafu Benedict XVI

2 Januari 2023

Kiongozi mstaafu wa Kanisa Katoliki, Benedict XVI alifariki Desemba 31, 2022 akiwa na umri wa miaka 95. Alipendwa na wengi, lakini pia alikosolewa na wengine.

https://p.dw.com/p/4LdSl
Papst Benedikt XVI
Picha: Patrick Hertzog/AFP/Getty Images

Benedict XVI ambaye jina lake halisi ni Joseph Aloisius Ratzinger alikuwa Mjerumani wa kwanza kuwa Papa takribani miaka 500 iliyopita. Hatua yake ya kujiuzulu Februari 28, 2013 ilikuwa ya kihistoria. Akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa takribani miaka minane, siku zote alisisitiza umuhimu wa hitaji la kiroho, pamoja na umuhimu wa Kanisa Katoliki katika ulimwengu wa kisasa ulioelimika.

Baada ya Makardinali kumchagua Mwadhama Joseph Kardinali Ratzinger aliyekuwa na umri wa miaka 78 kuchukua nafasi ya Papa John Paul II kuliongoza Kanisa Katoliki, kardinali huyo alitoka kwenye kibaraza cha Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter mjini Roma Aprili 19, 2005 na kusema: ''Makardinali wamenichagua mimi, mfanyakazi wa kawaida, mnyenyekevu katika shamba la mizabibu la bwana.''

Mhafidhina aliyesisitiza umuhimu wa huduma ya kichungaji

Papa Benedict XVI alikuwa mhafidhina, ambaye hata hivyo aliwashangaza wafuasi na wapinzani, hasa kwa sababu alikuwa mcha Mungu sana na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza. Papa huyo aliyesisitiza umuhimu wa huduma ya kichungaji, kwa hakika alihisi kufadhaishwa sana na mizozo mingi iliyolikumba Kanisa Katoliki wakati wa uongozi wake.

Papa Benedict XVI alizaliwa Aprili 16, 1927 katika jimbo la Bavaria, ambako baba yake alifanya kazi ya upolisi. Mwishoni mwa miaka ya 1950, Ratzinger aliheshimika kama profesa wa teolojia. Alipewa daraja la Upadri mwaka 1951, sawa sawa na kaka yake mkubwa George. Baada ya kuwa na uhusiano wa karibu na Askofu Mkuu wa Cologne, Josef Richard Frings, Ratzinger alihudhuria Baraza la Pili la Vatican kuanzia mwaka 1962 hadi 1965, ambapo alihutubia kuhusu uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na ulimwengu wa sasa.

Joseph Kardinal Ratzinger
Kardinali Joseph Aloisius Ratzinger (wa kwanza kulia aliyesimama) akiwa na wazazi wake (walioketi) pamoja na dada yake Maria (kushoto) na kaka yake George (katikati)Picha: Erzbistum/dpa/dpaweb/picture alliance

Mwaka 1997 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Munich na Freising na muda mfupi baadae kuwa Kardinali. Miaka minne baadae, Papa John Paul II alimpeleka Roma, ambako aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Kipapa la Mafundisho ya Imani. Wakatoliki wa Ujerumani walifurahi sana wakati Ratzinger alipochaguliwa kuwa papa mwaka 2005. Wengine walisema papa huyo alikuwa mzee sana kuliongoza kanisa, huku wengine wakiwa na wasiwasi kwamba uhafidhina wake unaweza kumfanya ashindwe kushinikiza mageuzi katika kanisa.

Kipindi cha mpito cha uongozi

Kwa mtazamo wa kisiasa, uongozi wake wa miaka minane ulikuwa wakati wa mpito, bado Papa Benedict XVI alitaka kuweka alama yake. Wakati wa kipindi chake cha kukikalia Kiti cha Mtakatifu Peter, pia aliwaweka wakfu zaidi ya nusu ya makardinali ambao badae mwezi Machi, 2013 walimchagua mrithi wake Papa Francis.

Papa Benedict hakuchoka kusisitiza mazungumzo kuhusu uhusiano kati ya dini na jamii ya kisasa. Mara nyingi alisisitiza imani yake kwamba Kanisa Katoliki linapaswa kuongoza Jumuiya ya Wakristo. Uhusiano wake na dini nyingine zisizo za Kikristo wakati fulani ulikuwa na mivutano.

Mhadhara wake mwaka 2006 huko Regensburg, Ujerumani, kwa mfano uliwaudhi wengi katika ulimwengu wa Kiislamu, kwani ulikuwa na nukuu ya kupotosha kuhusu Uislamu. Hata hivyo, baada ya muda hilo lilichochea mazungumzo kati ya viongozi wa kiroho wa Kikristo na Waislamu.

Kashfa ya unyanyasaji wa kingono

Uongozi wa Papa Benedict uligubikwa na ufichuzi kuhusu miongo kadhaa ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto wadogo, ambao ulifanywa na makasisi wa Kanisa Katoliki kwenye nchi kama vile Ireland, Marekani, Australia, Ubelgiji na hata Ujerumani. Wakosoaji baadae walilishutumu Kanisa kwa kukwepa kuchukua hatua stahiki kwa wahusika na badala yake liliwahamisha wahusika hao na kuficha uhalifu walioufanya. Hata hivyo, Papa Benedict alitaka kuliangazia suala hilo la kukosekana haki kwa wahanga na alikutana nao.

Vatikan Aufbahrung Papst Benedikt
Mwili wa Papa Mstaafu Benedict XVI ukiwa umehifadhiwa katika Monasteri ya Mama wa KanisaPicha: Vatican Media/ANSA/ZUMA Press/picture alliance

''Ninasikitishwa na mateso yaliyosababishwa na unyanyasaji wa watoto hasa ndani ya kanisa na wahudumu wake. zaidi ya yote ninaelezea masikitiko yangu makubwa kwa wahanga wasio na hatia wa uhalifu huu usioelezeka, pamoja na matumaini yangu kwamba kwa uwezo wa Neema ya Kristo, kujitoa kwake au upatanisho wake utaleta uponyaji wa ndani na amani katika maisha yao,'' alifafanua Benedict XVI.

Papa Benedict aliweka miongozo mikali ya kuwapatia mafunzo mapadri. Baada ya Papa Benedict kujiuzulu, ufichuzi zaidi wa kashfa za unyanyasaji wa kingono katika Kanisa Katoliki uliwekwa hadharani. Mwezi Februari, 2019, mrithi wake, Papa Francis aliitisha mkutano wa kilele wa Vatican kuzungumzia na kulishughulikia tatizo hilo.

Wengi washtushwa na kujiuzulu kwake

Uamuzi wa Papa Benedict kujiuzulu mwaka 2013 uliwashangaza wengi. Wakati wa miezi ya mwisho ya uongozi wake, akiwa na umri wa miaka 85, Papa Benedict alionekana mchovu. Hata hivyo, baadhi ya Wakatoliki walitegemea angeendelea kuliongoza Kanisa katoliki hadi kifo chake, kama ambavyo mapapa wengi walifanya kabla.

Baada ya kujiuzulu, Papa Mstaafu Benedict XVI alirejea mara moja tu Ujerumani, mwezi Juni, 2020 kwa ajili ya kumuaga kaka yake George aliyekuwa anaumwa pamoja na kusali katika makaburi ya wazazi wake huko Regensburg. Siku 10 baadae George alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 96. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 93, Papa Mstaafu Benedict XVI hakuweza kurejea Ujerumani kuhudhuria mazishi ya kaka yake.

(DW)