Mahakama yatoa waranti ya kukamatwa rais wa Korea Kusini
31 Desemba 2024Ofisi ya Uchunguzi wa Maafisa wa Ngazi za Juu (CIO) ilithibitisha kutolewa kwa waranti wa kumkamata Yoon siku ya Jumanne na Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi iliyoombwa na wachunguzi wanaochunguza sheria ya kijeshi iliyodumu kwa muda mfupi.
Yoon, ambaye kwa sasa amesitishwa kazi na bunge, anakabiliwa na uchunguzi kutokana na tuhuma kwamba alikuwa kiongozi wa uasi, mojawapo ya mashitaka ya uhalifu ambayo rais wa Korea Kusini hana kinga nayo.
Soma zaidi: Mahakama ya Korea Kusini yatoa waranti wa kukamatwa kwa Rais Yoon
Waranti huo wa kukamatwa kwa Yoon unaweza kutumika hadi tarehe 6 Januari na unawapa wachunguzi masaa 48 tu ya kumshikilia mwanasiasa huyo baada ya kumkamata. Baada ya hapo, wachunguzi wanapaswa ama waranti ya kumuweka kizuizini ama kumuachilia.
Mara tu akitiwa nguvuni, Yoon anatazamiwa kuwekwa kwenye Kituo cha Kuzuilia Watuhumiwa cha Seoul, kwa mujibu wa shirika la habari la Yonhap ambalo liliinukuu ofisi ya CIO.
Hata hivyo, wakili wa kiongozi huyo, Yoon Kab-keun, alisema waranti ya kumkamata mteja wake ulikuwa haramu na ulio kinyume na sheria kwa sababu CIO haikuwa na mamlaka kuomba waranti huo kwa mujibu wa sheria za Korea Kusini.
"Timu yetu ya wanasheria itawasilisha zuio kwenye Mahakama ya Katiba kuzuwia waranti huo," aliongeza wakili huyo.
Mkwamo wa kisiasa
Waranti wa kukamatwa kwa rais aliye madarakani ni jambo lililokuwa halikutegemewa na unaongeza mgogoro wa kisiasa ambao umeikumba Korea Kusini, taifa la nne kwa ukubwa wa kiuchumi barani Asia na mshirika mkuu wa Marekani.
Waziri Mkuu Han Duck-soo, anayekaimu nafasi ya Yoon, naye pia amepigiwa kura ya kutokuwa imani na bunge linalotawaliwa na upinzani.
Soma zaidi: Wabunge Korea Kusini wamuondoa rais wa pili katika wiki mbili
Waziri wa Fedha Choi Sang-mok, aliyechukuwa nafasi ya kaimu rais baada ya Han kuondolewa, amekuwa akishughulika na ajali ya ndege ya shirika la Jeju Air iliyotokea siku ya Jumapili (Disemba 29), ambayo iliuwa watu 179, ikiwa ajali mbaya kabisa kwenye ardhi ya Korea Kusini kuwahi kutokea.
Mamia ya wafuasi wa Yoon walikusanyika nje ya makaazi yake siku ya Jumanne kupinga waranti wa kukamatwa kwa kiongozi wao, huku wengine wakisukumana na polisi.
Katika tukio jengine tafauti, kesi yake ya kumuondowa madarakani ilikuwa inaendelea kusikilizwa kwenye Mahakama ya Katiba.