Mahakama ya Katiba Korea Kusini kuamua hatma ya Rais Yoel
16 Desemba 2024Majaji wote sita wa mahakama hiyo wanahudhuria mkutano huo wa kwanza juu ya uamuzi wa bunge wa kumwondoa Rais Yeol ambao ulipitishwa siku ya Jumamosi chini ya uongozi wa vyama vya upinzani.
Mahakama hiyo inao muda wa hadi miezi sita kutoa uamuzi wa iwapo Rais Yeol atavuliwa rasmi madaraka yake au kumrejesha mamlakani kuendelea kuliongoza taifa hilo.
Iwapo ataondolewa madarakani, uchaguzi mpya unapaswa kuitishwa ndani ya kipindi cha miezi miwili. Kufuatia kura ya bunge na mchakato wa mahakama, Rais Yeol, amewachia madaraka kwa muda na serikali ya nchi hiyo inaongozwa na Waziri Mkuu Han Duck-sooy.
Wakati huo huo shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap limeripoti kwamba wachunguzi nchini humo wanapanga kumhoji Rais Yeol mnamo wiki hii kuhusiana na jaribio lake lililoshindwa la kutangaza sheria ya kijeshi.
Duru zinasema mahojiano hayo huenda yafanyika siku ya Jumatano. Yeol pia bado yuko chini ya kizuizi cha kusafiri nje ya nchi wakati uchunguzi dhidi yake unaendelea.
Yumkini Rais Yeol na maafisa wengine wakashtakiwa kwa uasi dhidi ya dola
Kuna uwezakano kwamba Yeol na maafisa kadhaa waandamizi watakabiliwa na mashtaka ya uasi dhidi ya dola kutokana na tangazo la kiongozi huyo la tarehe 3 Disemba.
Waendesha mashtaka wamesema walikwishamwita mara ya kwanza kiongozi huyo kwa mahojiano lakini "amekataa kuitikia mwito huo" na sasa watatuma mwito mwingine.
Maandamano makubwa dhidi ya Yoon, pamoja na mikusanyiko midogo inayomuunga mkono, vimetikisa mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul, tangu amri yake ya sheria ya kijeshi.
Waandamanaji katika kambi zote mbili wameapa kuendeleza shinikizo huku Mahakama ya Katiba ikisubiriwa kuamua hatma ya Yoon.
Hapo jana Jumapili, Polisi waliwakamata wakuu wa sasa na wa zamani wa Kamandi ya Ujasusi ya Ulinzi kuhusiana na madai ya uasi, Yonhap iliripoti.
Waendesha mashtaka nao wamesema walikuwa wakitafuta hati ya kukamatwa kwa mkuu wa Kamandi Maalum ya Jeshi la Vita Kwak Jong-keun. Taarifa hizo ni kulingana na shirika la habari la Yonhap.
Kwak anatuhumiwa kutuma wanajeshi wa kikosi maalum bungeni wakati wa tangazo la sheria ya kijeshi lilipotolewa, hali iliyozusha makabiliano makubwa kati ya wanajeshi na wafanyakazi wa bunge.
Mkuu wa chama cha Rais Yeol kujiuzulu huku Korea Kaskazini ikitupa kijembe
Mkuu wa chama tawala cha Yoon People Power Party (PPP), ambaye hajahusishwa na tangazo la sheria ya kijeshi na ameonyesha kuunga mkono rais Yeol kuondolewa madarakani, amesema mapema leo kwamba atajiuzulu wadhifa wake.
"Ninaomba radhi kwa watu wote ambao wameteseka kutokana na tukio la tangazo la sheria ya kijeshi," Han Dong-hoon aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Seoul.
Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini leo Jumatatu vimeshambulia Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol vikimtaja kuwa "kiongozi wa uasi". Hayo yalikuwa matamshi ya kwanza tango Yeol alipoondolewa madarakani
Serikali mjini Pyongyang imejizuia kutia neno katika msukosuko wa kisiasa wa Korea Kusini, ambao ulifikia kilele siku ya Jumamosi pale bunge la nchi hiyo lilipopiga kura ya kumwondoa madarakani Rais Yeol kwa "uasi".
Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) liliripoti kuwa Yoon amejaribu kuepusha zahma ya kile limekitaja kwua "tangazo la kipumbavu la sheria ya kijeshi" kwa vyama vya upinzani.
"Uchunguzi dhidi ya kibaraka Yoon Suk Yeol, kiongozi wa uasi, na washirika wake unaendelea," limeripoti shirika la KCNA ilisema.
Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini mara nyingi huwataja viongozi wa Korea Kusini kuwa "kibaraka" wa mshirika wake wa jadi, Marekani.