1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Tanzania yataka marekebisho ya sheria ya ndoa

Veronica Natalis
22 Juni 2023

Mahakama kuu ya Tanzania Masijala ya Dar es Salaam imeipa serikali ya nchi hiyo miezi sita ya kutekeleza maamuzi ya mahakama yanayohusu marekebisho ya sheria ya ndoa juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa.

https://p.dw.com/p/4SvTK
Tansania - AGAPE Frauenkollektiv - Proteste von Schülerinnen
Picha: DW/V. Natalis

Chini ya wakili  wa kujitegemea John Seka, shirika la kutetea maslahi ya wanawake na watoto, WOCWELS, lilifungua kesi hiyo katika Mahakama kuu ya Tanzania masijala ya Dar Es Salaam, likipinga mchakato wa serikali kupitia wizara ya katiba na sheria wa kukusanya maoni kuhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa, huku katika dodoso la maoni hayo wizara ikiutaja umri wa mtoto wa kike kuolewa kuwa ni miaka 14. Kesi hiyo ya shirika la WOCWELS iliyofunguliwa mwaka jana 2022, iliitaka Mahakama kusitisha mchakato huo na badala yako wizara ya katiba na sheria ipeleke muswada wa bungeni, wa marekebisho ya sheria ya ndoa Tanzania ya mwaka 1971. Merry Mushi ni mkurugenzi wa shirika hilo.

Msichana mwanaharakati dhidi ya ndoa za utotoni Tanzania

Mwaka 2016, Makama kuu ya Tanzania  ilimpa ushindi mwanaharakati Rebeca Gyumi aliyekuwa akipinga baadhi ya vifungu katika sheria ya ndoa nchini Tanzania, inayohalalisha mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14.

Kwenye kesi ya mwanaharakati Rebeca Gyumi iliamriwa  kwamba umri wa mtoto kuolewa uwe ni miaka 18 na serikali ikakata rufaa kwa sababu haikuridhika na uamuzi huo lakini hata hivyo ilishindwa na sheria ilitakiwa kubadilishwa.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wizara ya sheria na katiba ilianza kukusanya maoni  ya wadau kuhusu umri wa mtoto wa kike  kuolewa, badala ya kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria hiyo bungeni. Nimemuuliza Wakili John Seka aliyesimamia kesi ya shirika la WOCWELS anadhamu maamuzi yaliyotolewa na Mahaka safari hii yatatekelezwa.

Mbali na kutolewa maamuzi hayo, lakini pia mahakama imekea mwenendo wa serikali ya Tanzania kusita sita ama kutotekeleza baadhi ya maamuzi ya Mahakama za ndani na za kimataifa. Veronica Natalis, DW Arusha.