1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Angola yahalalisha ushindi wa chama tawala

Hawa Bihoga
6 Septemba 2022

Mahakama ya katiba nchini Angola imetupilia mbali madai ya upinzani kufuta matokeo ya uchaguizi mkuu ambayo yalikipa ushindi chama tawala cha MPLA kwa asilimia 51 dhidi ya upinzani uliopata asilimia 44.

https://p.dw.com/p/4GTDr
Angola Wahl 2022, UNITA-Pressekonferenz
Picha: A. Cascais/DW

Mahakama ya katiba nchini Angola imetupilia mbali madai ya upinzani kutaka kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu ambayo yalikipa ushindi chama tawala cha MPLA kwa asilimia 51 dhidi ya upinzani uliopata asilimia 44.

Umoja wa Kitaifa wa Uhuru Kamili wa Angola, UNITA, uliwasilisha malalamiko kwenye mahakama ya kikatiba nchini humo, kwa kutangazwa kwa vuguvugu la muungano wa ukombozi wa Angola MPLA kama mshindi wa uchaguzi huo.

Hata hivyo mahakama imeamuru kwamba malalamiko ya upinzani hayana mashiko kiasi kuruhusu malalamiko hayo kubatilisha matokeo.

UNITA imetumia utaratibu huo uliowekwa kisheria ili kulinda haki ya kikatiba lakini mahakama iliamuru kufutilia mbali malalamiko hayo hatua inayoruhusu mchakato wa kidemokrasia kuendelea.

Matokeo ya tume ya uchaguzi wiki iliopita yalikipa chama tawala cha MPLA ushindi wa asilimia 51.17 ya kura na upinzani UNITA walipata asilimia 44.

Kulingana na ujumuishwaji wa matokeo uliofanywa na upinzani unadai, UNITA ilipata asilimia 49.5 ya hesabu ya kura na chama tawala MPLA kilipata asilimia 48.2.

Soma zaidi:MPLA yashinda uchaguzi Angola

Kiongozi wa chama cha upinzani Adalberto Costa Junior katika mkutano wake na waandishi wa hababri amesema kwamba wamebaini udanganyifu mkubwa baada ya ujumuishwaji wa kura ikilinganishwa na tume ya uchaguzi Angola CNE.

Amesema kiasi cha kura 347,436 ziliibwa kutoka UNITA katika majimbo 15 ya uchaguzi, wakati kura 185,825 ziliongezwa kwa chama tawala MPLA katika majimbo 16 ya ubunge.

Katika hatua nyingine Adriano Abel Sapinala ambae ni kiongozi wa UNITA katika jimbo la Benguela amesema wafuasi 10 wa chama chake walijeruhiwa vibaya wakati wafuasi wa MPLA walipovamia na kushambulia ofisi za chama hicho huko Bocoio.

Rais Lourenco: Waangola wameshaamua

Rais wa Angola Joao Lourenço amesema kwamba tayari wananchi wamekwishaaamua na wanahitaji kukiona chama tawala MPLA kikiwaongoza kwa awamu nyingine ya miaka mitano.

Angola | MPLA | Präsident Joao Lourenco
Rais wa Angola Joao Lourenço akiwa katika jukwaa la kisiasaPicha: Adolfo Guerra/DW

"Waangola wameshaamua, kama ilivyokuwa kufanya jukumu lao wamefanya"

Soma zaidi:Raia wa Angola wapiga kura katika kinyang'anyiro kikali

Alisema na kuongeza kwamba raia wanaitaka serikali ya MPLA kwa miaka mingine mitano ijayo, kama hakikisho la utulivu.

"Wanahitaji utulivu na uimarishaji wa serikali ya kidemokrasia kwa kuzingatia utawala wa sheria." Alisema rais Lourenco.

Ushindani mkali washuhudiwa kwenye uchaguzi

MPLA kimekuwa chama pekee kutawala nchi hiyo tangu kilipojinyakulia uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Angola Luanda | Polizei verhindert Pressekonferenz in Cazenga
Raia wa AngolaPicha: A. Cascais/DW

Hata hivyo katika uchaguzi wa awamu hii chama hicho kilikabiliwa na wakati mgumu kutokana na ushindanimkali ulioshuhudiwa kutoka chama cha upinzani, ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017 ilipojipatia ushindi wa asilimia 61.

Soma zaidi:Lorenco tena Angola

Angola ambalo ni taifa la pili barani Afrika kwa usafirishaji wa mafuta ghafi, lakini rushwa na upendeleo zimelifanya taifa hilo maendeleo yake kwenda kwa mwendo wa pole.

Uchaguzi uliomalizika uligubikwa na hoja ya kufufuliwa kwa uchumi ambao unasuasua, mfumko wa bei kwa bidhaa na huduma na umasikini unaoshuhudiwa miongoni mwa wananchi wengi ambao wanaishi chini ya dola mbili kwa siku.