1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli aruhusu vyuo, michezo kuanza tena

George Njogopa21 Mei 2020

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametangaza kuwa vyuo vikuu nchini humo vitafungufuliwa Juni Mosi, na kuruhusu pia shughuli zote za michezo nazo ziendelee kama kawaida.

https://p.dw.com/p/3cZr3
Präsident John Magufuli aus Tansania
Picha: Reuters/T. Mukoya

Rais Magufuli amesema vyuo vikuu vyote sasa vitarejea katika hali yake ya kawaida kuendelea na masomo kuanzia Juni Mosi baada ya kijiridhisha kutokana na maendeleo ya hali ya maambukizi ya virusi vya corona.

Amesema maambukizi nchini humu yameshuka kwa kiwango cha kuridhisha hatua ambayo imemfanya aanze kufungua baadhi ya shughuli zilizokuwa zimesimama kutokana na janga hilo la virusi vya corona lilipopiga hodi kwa mara ya kwanza nchini Machi 16.

"Ikiwa mwelekeo nnaouona utandelea katika wiki zijazo, napanga kufungua vyuo vikuu ili wanfunzi waendelee na masomo yao, alisema Magufuli wakati akizungumza kwenye ibada ya misa kaskazini-magharibi mwa nchi wiki iliyopita.

Hatua nyingine ambazo Rais Magufuli amezitangata wakati alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni ni kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha sita wanaojiandaa na mitihani ya kuhitimu masomo yao kurejea shuleni.

Amesema wanafunzi hao watarejea kwenye masomo yao kuanzia Juni Mosi na kwamba mamlaka zinazohusika na masuala ya taalamu zitawajibika kuandaa mpango ili kuwawezesha wanafunzi hao kufidia muda wa masomo walioukosa.

Einweihung des neuen Flughafen Terminals: Julius Nyerere International Airport  in Dar es salaam Tansania
Rais Magufuli akipiga push up katika moya ya matukio yake ya kisiasa.Picha: DW/E. Boniphace

Mamlaka kuweka kanuni kanuni za afya michezoni

Kuhusu suala la michezo, Rais Magufuli ambaye pia amekuwa akihimiza kutumia njia za asili kukabiliana na maambukizi ya COVID-19 amesema ingawa ameruhusu michezo yote kurejea tena kuanzia Juni Mosi, mamlaka zinazohusika zitapaswa kuweka utaratibu ukaozingatia kanuni za kiafya.

Tanzania pia imefungua anga yake kwa ajili ya kuruhusu ndege za kibiashara na imesema watalii wanaotaka kuja nchini wanaweza kufanya hivyo kuanzia Mei 27 na hakutakuwa na karantini yoyote.

Kwa kuruhusu kufunguliwa kwa vyuo vikuu pamoja na kurejea kwa shughuli za kimichezo, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na eneo la Afrika Mashariki kufanya hivyo wakati mataifa mengine katika eneo hilo yakiendelea na marufuku zilizowekwa kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwa muda sasa Tanzania imekuwa kitovu cha mjadala unaoendelea duniani jinsi inavyolishughulikia janga la virusi vya corona wakati taifa hili likisisitiza kwamba pamoja na kuzingatia kanuni za kiafya, jambo la kumtegemea Mungu ndiyo nguzo kubwa katika kuishinda vita hiyo.