Mafuriko yawaua zaidi ya watu 1,000 huko Pakistan
29 Agosti 2022Mamlaka ya taifa inayoshughulikia maafa nchini Pakistan imeripoti jana kwamba watu 1,061 wakiwemo watoto 348 wamefariki dunia tangu kuanza kwa msimu wa mvua za masika katikati ya mwezi Juni. Mvua hizo zimesababisha mafuruko makubwa yaliyosomba vijiji na mazao, huku wanajesi na wafanyakazi wa uokoaji wakiendelea na juhudi za kuwanusuru watu waliokwama.
Mafuriko kutoka mto Swat yameathiri jimbo la kaskazini magharibi la Khyber Pakhtunkhwa ambako maelfu ya raia hususan katika wilaya za Charsadda na Nowshehra walikuwa wameondolewa kutoka majumbani mwao na kupelekwa kwenye makambi ya misaada yaliyowekwa katika majengo ya serikali. Wakaazi wengi pia wamejihifadhi kando ya barabara.Pakistan yahitaji misaada ya dharura
Msimu huo wa mvua za masika ambao haujashuhudiwa kwa muda mrefu umeathiri majimbo yote manne ya nchi. Nyumba takribani laki 300,000 zimeharibiwa, barabara nyingi hazipitiki na umeme umekatika na kuathiri mamilioni ya wakaazi. Serikali imesambaza askari kusaidia mamlaka za kiraia katika zoezi la uokoaji na utoaji wa misaada kote nchini.
Jeshi la Pakistan limesema pia katika taarifa yake kwamba limefanikiwa kuwaokoa watalii 22 waliokuwa wamekwamba katika bonde kaskazini mwa nchi. Waziri mkuu wa Pakistan Shabaz Sharif amewatembelea wahanga jimboni Baluchistan na kuahidi kwamba serikali itatoa makaazi kwa wote walioathirika. Serikali ya Pakistani imetangaza hali ya dharura ya kitaifa na kutoa wito wa msaada wa kimataifa.Waathirika wa mafuriko Pakistan wakabiliwa na njaa na magonjwa
Maafisa wanasema mamilioni ya watu wakiwemo watoto wako katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya mlipuko katika mikoa iliyokumbwa na mafuriko. Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Bilawal Bhutto-Zardari amesema nchi hiyo inahitaji usaidizi wa kimataifa kuweza kukabiliana na athari za mafuriko hayo makubwa.
"Sijaona uharibifu wa kiwango hiki, naona vigumu sana kuelezea kwa maneno ambayo tumezoea, iwe ni mvua za masika au mafuriko, haionekani kuwa ya kawaida kwa uharibifu na maafa yanayoendelea ambayo bado tunayashuhudia."
Kulingana na waziri huyo wa mambo ya nje, Pakistan itazindua wiki hii kampeni ya kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchangia katika juhudi za misaada, huku nchi hiyo ikitizama jinsi ya kushughulikia athari za muda mrefu za mabadiliko ya tabia nchi. Taifa hilo la kusini mwa Asia tayari lilikuwa likikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi, mfumuko mkubwa wa bei na kushuka kwa thamani ya sarafu.