Maelfu ya watu Msumbiji wamlaki Mondlane aliporejea
9 Januari 2025Maelfu ya watu nchini Msumbiji wamejitokeza kumlaki kiongozi mkuu wa upinzani wa Msumbiji Venancio Mondlane, aliyekuwa anarejea baada kukaa uhamishoni kwa zaidi ya miezi miwili ili kushinikiza madai yake kwamba alishinda uchaguzi wa rais wa Oktoba 9 mwaka uliopita.
Kiongozi huyo wa upinzani amewasili Msumbiji mapema Alhamisi akitokea uhamishoni. Maelfu wa raia walikusanyika kumlaki kiongozi huyo ingawa vikosi vya usalama viliwazuia wafuasi wake hao kwenda kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Maputo kukutana na Venancio Modlane alipokuwa akitua.
Vurumai hilo kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Mondlane vimesababisha kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi, hayo yamesemwa la shirika la habari la Ufaransa, AFP.
Lakini maelfu walikusanyika baadaye kwenye soko lililopo katikati mwa jiji la Maputo wakiimba "Venancio" na kupiga filimbi na vuvuzela huku Mondlane akiwa ameambatana na walinzi, akisimama juu ya gari na kupunga mkono na kuusalimia umati huo.
Soma pia: Kiongozi wa upinzani Msumbiji arejea nchini kutoka uhamishoni
Mwandishi wa shirika la habari la AFP amesema gari la kiongozi huyo wa upinzani lilizingirwa na umati mkubwa wa watu huku polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi kutuliza hali na kuwatawanya watu hao.
Kurejea kwa Mondlane kunajiri wiki moja kabla ya kuapishwa kwa rais ajaye, Daniel Chapo, mgombea wa chama tawala cha Frelimo ambaye alitangazwa mshindi wa kura.
Mondlane: Kura ziliibiwa
Mondlane anadai kura ziliibwa na kukipendelea chama tawala cha Frelimo ambacho kimeitawala nchi tangu uhuru kutoka kwa ureno mwaka 1975.
Akiwa katika uwanja wa ndege kiongozi huyo wa upinzani aliweka kiapo mbele ya kamera za wanahabaari, akiwa na Biblia mkononi na kujitambulisha kama 'Rais aliyechaguliwa na watu wa Msumbiji.'
''Mimi, Venancio Mondlane, rais niliyechaguliwa na watu wa Msumbiji, sio na baraza la katiba, sio na CNE, lakini niliyechaguliwa kwa mapenzi ya kweli ya watu, ninaapa kwa heshima yangu kwamba nimeitumikia nchi ya Msumbiji na watu wa Msumbiji.''amesema Mondlane.
Soma zaidi: Zaidi ya wafungwa 1,500 watoroka Msumbiji
Kwa mujibu wa masharika ya kutetea haki za binadamu katika eneo hilo, mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi nchini Msumbiji umeidumbukiza nchi hiyo katika ghasia na kusabibisha vifo vya takribani watu 300, wakiwemo waandamanaji waliouawa katika msako mkali wa polisi.
Machafuko hayo yamesababisha hasara kubwa kwa uchumi wa Msumbiji,na kusimamisha biashara ya mipakani. Usafirishaji wa meli, madini na viwanda pia vimeathiriwa, huku maelfu ya watu wakiripotiwa kukimbilia nchi jirani.
Kiongozi huyo wa upinzani amesema amerejea nchini mwake "kushuhudia" kile alichosema ni mashambulizi na utekaji nyara wa wafuasi wake na kujibu mashtaka yoyote ya jinai ambayo mamlaka imeweka dhidi yake.
Hata hivyo, serikali imetoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kuumaliza mzozo, huo lakini ikapuuza ombi la Mondlane la kutaka mazungumzo hayo yafanyike kwa njia ya mtandao alipokuwa nje ya nchi.