1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia hujuma za vikosi vya Urusi Idlib

Oumilkheir Hamidou
15 Januari 2020

Ndege za kivita za Urusi zimehujumu miji kadhaa ya mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib unaodhibitiwa na waasi, kwa mara ya kwanzatangu makubaliano ya kuweka chini silaha pamoja na Uturuki yalipoanza kufanya kazi

https://p.dw.com/p/3WDzE
Syrien Binnish Angriffe auf syrisches Rebellengebiet
Picha: picture-alliance/dpa/A. Alkharboutli

Waasi na mashahidi wanasema miji ya Khan al Subi, Maasaran na miji mengine kadhaa ya kusini mwa mkoa wa Idlib, ngome ya mwisho ya waasi, ilihujumiwa upya baada ya siku mbili tu za utulivu ."Ndege za kivita za Urusi zimevuruga hali ya utulivu  iliyowaruhusu watu kupumuwa kidogo kwa siku mbili baada ya hujuma za kila siku" amesema mwanaharakati mmoja anaejitambulisha kama "Mohammed Rashid.

Malaki ya watu wameuhama mkoa wa Idlib mnamo wiki za hivi karibuni baada ya ndege za kivita za Urusi na zile za serikali ya Syria kuhujumu miji na vijiji kadhaa kufuatia wimbi jipya la mashambulio ya serikali yaliyolengwa kuwatimua waasi toka eneo hilo.

Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa walisema mapema mwezi huu kwamba hali ya kiutu imezidi kuwa mbaya huku watu wasiopungua laki tatu wakiupa kisogo mkoa wa Idlib, wakijiunga na wengine laki tano ambao tayari wamepiga kambi karibu na mpaka wa Uturuki.

watu wanaongozana katika eneo la kati la Idlib
watu wanaongozana katika eneo la kati la IdlibPicha: picture alliance/AP/G. al-Sayed

Ujia salama wafunguliwa

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hujuma hizi za sasa za ndege za kivita za Urusi zimelengwa karibu na yale maeneo ya mkoa wa Idlib ambako karibu watu milioni tatu wamekwama, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Viongozi wa mjini Moscow wanasema wanajeshi wao pamoja na wale wa Syria na kwa ushirikiano pamoja na wanamgambo wanaungwa mkono na Iran wanazuwia mashambulio ya kigaidi ya wafuasi wa itikadi kali wa Alqaida dhidi ya raia wanaoishi katika maeneo yanayodhdibitiwa na serikali.

Kambi za wakimbizi karibu na mpaka wa Uturuki
Kambi za wakimbizi karibu na mpaka wa UturukiPicha: picture-alliance/AA/E. Turkoglu

Mikururo ya watu wakimbilia karibu na mpaka wa Uturuki

Mapema  wiki hii viongozi wa mjini Moscow walisema wamefungua "njia salama" kuwaruhusu watu wanaoishi katika maeneo yanayosimamiwa na upande wa upinzani katika mkoa wa Idlib kukimbilia katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Wakaazi wanasema watu wachache tu ndio walioitumia fursa hiyo na kuingia katika maeneo yanayodhiitiwa na serikali ambako wanahofia kuadhibiwa, wengi wameelekea katika maeneo ya karibu na mpaka wa Uturuki.