1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Madagascar kupinga sheria za uchaguzi

23 Aprili 2018

Maelfu ya wafuasi wa upinzani nchini Madagascar wamerudi mitaani kupinga dhidi ya rais na ukandamizaji mbaya wa vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya kuipinga serikali, ambamo watu wawili waliuawa mwishoni mwa wiki.

https://p.dw.com/p/2wW35
Madagaskar Demonstration der Opposition in Antananarivo
Picha: Getty Images/AFP/Rijasolo

Rais wa Madagascar alilaani maandamano hayo siku ya Jumapili na kuyaita mapinduzi, na kuwaonya wale aliowaita wafanya vurugu dhidi ya kuendelea na maandamano hayo.

"Natoa wito kwa watu wote wa Madagascar kuwa watulivu, kuheshimu demokrasia, lakini kilichotokea Jumamosi si kingine bali ni mapinduzi," alisema rais Hery Rajaonarimampianina katika hotuba kwa njia ya televisheni, akizungumzia makabiliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji wa upinzani.

"Tunapaswa wote kushawishika kwamba mapinduzi hayaleti suluhisho kwa mustakabali wa taifa letu. Nawaonya wafanya fujo na wale wanaong'ang'ania chuki na makabiliano wakitafuta umuagaji damu na upotevu wa maisha," aliongeza.

Siku ya Jumapili vikosi vya usalama vilipiga marufu watu kuingia katika uwanja wa May 13 katikati mwa mji mkuu Antananarivo wakati wa majira ya asubuhi, kabla ya kuondoka na kuwaruhusu waandamanaji kukusanyika kwa amani.

Bildergalerie Herausforderungen für Madagaskars neuen Präsidenten Hery Rajaonarimampianina
Rais Hery Rajaonarimampianina ameyaeleza maandamano ya upinzani kuwa ni "mapinduzi."Picha: DW/P. Hille

"Ili kuepusha makabiliano, ambayo yangesababisha uharibifu mkubwa kati ya Wamadagascar, tuliamua kuondoka katika eneo ambalo hapo awali tulikuwa tumelilinda," alisema waziri wa ulinzi Jenerali Beni Xavier Rasolofonirina wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya maandamano ya Jumatatu.

Lakini aliwaonya waandamanaji kwamba "kamwe polisi haitaruhusu madaraka yasiotokana na mchakato wa uchaguzi, kwa sababu hicho ndicho kinachoendana na katiba."

Mahasimu Ravalomanana, Rajoelina waungana

Waandamanaji wamekuwa wakiandamana dhidi ya sheria mpya za uchaguzi, ambazo wapinzani wanadai huenda zikawazuwia baadhi ya wagombea kushiriki katika uchaguzi ujao wa rais.

Kisiwa hicho kikubwa kilichoko katika bahari ya Hindi, ambacho kimekumbwa na miongo kadhaa ya machafuko ya kisiasa, kinatarajia kufanya uchaguzi mwishoni mwa mwezi Novemba au Desemba.

Serikali ilikuwa imeyatangaza maandamano ya Jumamosi kuwa kinyume na sheria, lakini karibu wanaharakati 1,000 wa upinzani walikaidi amri hiyo na vikosi vya usalama vilitumia hewa ya kutoa machozi kutawanya makundi.

Wafausi wa mwanasiasa wa upinzani, Marck Ravalomanana, kiongozi wa zamani wa taifa hilo, wanasema sheria mpya za uchaguzi zimetengenezwa ili kumzuwia kuwania katika uchaguzi huo. Upinzani pia unapinga vipengele kuhusu ufadhili wa kampeni na matumiazi ya vyombo vya habari katika sheria hizo.

Madagaskar Ex-Präsident Marc Ravalomanana
Rais wa zamani wa Madagascar Marc Ravalomanana, ambaye wafuasi wake wanasema sheria mpya za uchaguzi zinalenga kumzuwia asigombee urais.Picha: picture-alliance/dpa

"Tunapinga sheria hizo zilizopitishwa na wabunge mafisadi," alisema Christine Razanamahasoa, mbunge wa upinzani.

Ravalomanana, alieondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2009, ameungana na mtu aliemrithi, Andy Rajoelina, kupinga sheria hizo zilizoshinikizwa na rais Hery Rajaonarimampianina.

Rajaonarimampianina, aliechaguliwa mwaka 2013, hajasema bado iwapo atawania muhula mwingine.

Wito wa utulivu na kujizuwia

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Madagascar, umewatolea mwito wanasiasa nchini humo kujizuwia, na umeelezea uungaji wake mkono kwa uchaguzi wa "kuaminika, wa uwazi na shirikishi mwaka 2018."

Mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Madagascar, Ahmed Youssouf Hawa, pia alitoa wito wa utulivu, kujizuwia na uwajibikaji.

"Madagascar haihitaji kutumbukia tena katika hali ngumu miezi michache tu kabla ya uchaguzi," alisema katika taarifa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.

Mhariri. Saumu Yusuf