1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya dharura vyaendelea kuwasaka manusura, Libya

15 Septemba 2023

Vikosi vya dharura leo vinaendelea kutafuta manusura zaidi baada ya maelfu ya watu kutangazwa kuwa hawajulikani waliko kufuatia mafuriko makubwa yalioukumba mji wa bandari wa Derna nchini Libya.

https://p.dw.com/p/4WN9S
Operesheni za kuwaokoa wahanga wa mafuriko kutokana na kimbunga Daniel nchini Libya imeendelea, ingawa matumaini yanazidid kufifia kila siku
Operesheni za kuwaokoa wahanga wa mafuriko kutokana na kimbunga Daniel nchini Libya imeendelea, ingawa matumaini yanazidid kufifia kila siku Picha: Hamza Al Ahmar/AA/picture alliance

Umoja wa Mataifa umeyataja mafuriko hayo kuwa "janga" na umetoa wito wa zaidi ya dola milioni 71 ili kusaidia zaidi ya watu 250,000 kati ya 884,000 wanaoorodeshwa kuwa na uhitaji mkubwa.

Muuguzi Mona Talib Khaled amesema "Tunajitolea kuwaokoa ndugu zetu katika mji wa Derna, na kwa msaada wa Mungu, tutajitahidi na kuwaleta ndugu zetu kwenye maeneo salama. Mtu anapoona janga kama hili, kama binadamu lazima ahisi uchungu wa ndugu zake. Mtu yeyote anaweza kujitolea badala tu ya kubaki nyumbani."

Shirika la Hilali Nyekundu la Libya limesema watu 11,300 wamepoteza maisha na wengine 10,100 hawajulikani waliko.

Kimbunga Daniel kimeua watu 170 katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Waziri wa afya wa serikali ya mashariki mwa Libya Othman Abduljaleel ameeleza kuwa, watu waliopoteza maisha wamezikwa kwenye makaburi ya halaiki nje ya mji ya Derna na miji mengine ya karibu.