1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko ya Kenya Magazetini

21 Novemba 2014

Machafuko katika mji wa Mombasa, Kenya kati ya vikosi vya polisi na wafuasi wa itikadi kali,vurugu katika bunge la Afrika kusini na fainali za kombe la mataifa barani Afrika ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/1Dr9E
Polisi wameingia msikitini Kisauni na kuwakamata watuhumiwaPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini Afrika Mashariki nchini Kenya ambako machafuko makali yameripotiwa wiki hii kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam. Duru za hadi hivi karibuni zinasema watu wasiopungua wanne waneuwawa. Chanzo cha machafuko hayo ni msako wa polisi katika misikiti miwili ya mji huo-Msikiti Musa na Msikiti Sakina inayoangaliwa kama vituo vya kuwaandikisha watu wanaotaka kujiunga na wanamgambo wa kigaidi wa Al Shabab nchini Somalia,linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Kujipenyeza wafuasi wa itikadi kali katika mji huo wa mwambao si jambo geni linakumbusha gazeti hilo linalosema tangu muda mrefu uliopita mashekhe wa kigeni wamekuwa wakiingia katika mji huo wa mwambao na kuahidi miongoni mwa mengineyo kutoa fedha za Saud Arabia kuitengeneza upya misikiti hiyo ili badala yake waruhusiwe kutuma maimam ambao hatimae hutoa mawaidha yanayohimiza jihad. Kwa muda mrefu mawaidha hayo hayakuwa yakisaidia kwasababu idadi kubwa ya waislam katika mji huo wa mwambao wa Kenya hawafuati itikadi kali na wanawachukulia kwa tahadhari pia maimam kutoka nje.Frankfurter Allgemeine linasema tangu miaka minne iliyopita wanaotoa mawaidha ya kupalilia chuki na kutovumiliana mjini Mombasa ni maimam wazaliwa wa Kenya. Wote wamesomea Saud Arabia. Frankfurter Allgemeine limetoa mifano ya maimam mfano wa Abubakar Shariff Ahmed,aliyekuwa akijulikana mashuhuri kama Makaburi,Sheikh Aboud Rogo aliyeuliwa Agosti mwaka 2012 na Shiekh Ibrahim Omar aliyekamata nafasi yake na kuuliwa pia octoba mwaka jana. Aboubakar Shariff Ahmed aliyeshika nafasi ya Sheikh Omar linaandika Frankfurter Allgemeine ameuliwa pia april mwaka huu. Mauwaji yote hayo mpaka leo haijulikani yamefanywa na nani. Na kila kisa cha mauwaji kimefuatiwa na mauwaji ya kulipiza kisasi na wanaoathiorika zaidi linaaendelea kuandika Frankfurter Allgemeine ni waislam wanaofuata imani ya wastani,likitoa mfano wa Sheikh Mohammed Idriss aliyeuliwa akiwa ndani ya gari yake mwezi juni mwaka huu. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linamaliza kwa kusema hata wageni,akiwemo mtalii mmoja wa kijerumani, wamekuwa pia wakiangukia mhanga wa wafuasi wa itikadi kali na mpaka leo "wahalifu hawajapatikana."

Vurugu Afrika Kusini

Die Tageszeitung limeandika kuhusu vurugu zisizokwisha katika bunge la Afrika kusini. Wawakilishi wa chama tawala cha ANC na wale wa upande wa upinzani wanazozana kuhusu tabia za rais Jacob Zuma-Kunazuka mapigano na polisi kuingilia kati, linaandika gazeti hilo la mji mkuu linaloashiria spika wa bunge la Afrika kusini Beleka Mbete ambae tayari ameshajikuta akihujumiwa kwa maneno na upande wa upinzani,hatokuwa na hazi rahisi kikao chengine cha bunge kitakapofunguliwa jumanne ijayo. Upande wa upinzani hautaki kuyatambua madaraka ya spika huyo wa bunge tangu pale polisi ilipoingilia kati bungeni alkhamisi iliyopita na kuwatoa wabunge waliokuwa wakiasi wa upande wa upinzani.

Chanzo cha mzozo huu wa sasa ni hali ya kuvunjika moyo dhidi ya chama tawala cha ANC na rais Jacob Zuma wa Afrika kusini. Upande wa upinzani na hasa chama kikuu cha upinzani cha Muungano wa Demokrasia DA na kile kipya cha EEF unamtuhumu rais Zuma hataki kuhudhuria hadhara kuu ya bunge ili kukwepa kujieleza kuhusu ukarabati wa nyumba yake katika mji alikozaliwa wa Nkandla katika jimbo la Kwazulu Natal,akitumia fedha za wananchi zisizopungua Euro milioni 17. Tangu mwisho wa mwezi wa Agosti rais Zuma hajahudhuria kikako cha bunge-wakati ule wabunge wa chama cha EEF walimtaka arejeshe fedha hizo.

Mashabiki wa dimba Afrika kurejea Guinea ya Ikweta

Na mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu uamuzi wa shirikisho la kabumbu barani Afrika CAF kuhamishia Guinea ya Ikweta fainali za kombe la mataifa 2015 baada ya Moroko kukataa kuandaa mashindano hayo kwa hoja za kitisho cha maambukizo ya maradhi hatari ya Ebola. Frankfurter Allgemeine linaandika Mashabiki wa Dimba barani Afrika wanajikuta wakilazimika kurejea kwa muimla Teodoro Obiang.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Mohammed Khelef