Maandamano yaitishwa Tunisia kupinga kifo cha kiongozi wa upinzani
26 Julai 2013Maduka na Mabenki yamefungwa huku Shirika la ndege la Tunisia, Tunisair likifuta safari zake zote hii leo kutokana na maandamano yaliyopangwa kufanyika mjini Tunis kufuatia madai kwamba serikali imehusika na mauaji ya kiongozi huyo wa upinzani Mohamed Brahmi.
Brahmi mwenye umri wa miaka 58 na aliyekuwa katika vuguvugu la wanasiasa wa mrengo wa shoto aliuwawa nje ya nyumba yake mjini Ariana na watu wasiojulikana.
"Alipigwa risasi mbele ya mke wake na watoto," Alisema Mohsen Nabti, mwanachama wa vuguvugu analotokea Brahmi.
Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini humo mwanae kiongozi huyo kwa jina Aden alisikia mlio wa kwanza wa risasi kisha mlio mwengine uliofuatiwa na milio mengine kadhaa nje ya nyumba yao.
Baadaye yeye na dadake wakakimbia nje kuona kilichokuwa kinaendelea na hapo ndipo walipoliona gari la baba yao huku watu wawili wakitoroka kwa kutumia pikipiki.
Maandamano muda mchache baada ya mauaji
Baada ya kuenea kwa habari hizo za mauaji, maandamano yakazuka mjini Tunis na katika mji wa Sidi Bouzid, eneo ambalo ni kitovu cha maandamano ya kutaka mageuzi yaliyofanyika miaka kadhaa iliopita.
Hata hivyo polisi walijaribu kuwatawanya waandamanaji kwa kuwarushia gesi za kutowa machozi. Waandamanaji hao walikuwa wameshaanza kujiwekea makambi ya kuanza maandamano ya kutaka kuondoka kwa utawala wa sasa.
Baada ya mauaji ya jana waziri mkuu wa Tunisia Ali Larayedh, aliwaambia waandishi habari kwamba analaani mauaji hayo ya kinyama yanayolenga kuyumbisha usalama wa nchi.
Kwa upande wake Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Tunisia umeitisha maandamano makubwa kufanyika leo kupinga visa vya kigaidi na mauaji ya kiholela yanayotokea nchini humo.
Mauaji ya Mohamed Brahmi yamefanyika miezi sita baada ya kiongozi mwengine wa upinzani Chokri Belaid kuuwawa katika mazingira sawa na hayo. Mauaji ya Chokri pia yalidaiwa kutekelezwa na chama tawala cha Ennahda.
Serikali yakanusha kuhusika na mauaji
Hata hivyo chama hicho kupitia mkuu wake Rached Ghannouchi kimekana vikali kuhusika na mauaji yote mawili.
Ghannouchi amesema mauaji ya Brahmi ni jambo la kusikitisha kwa taifa zima huku akisema kwamba wale wanaohusika na mauaji kama hayo wanataka kuiingiza Tunisia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuvuruga kipindi cha mpito kinachozingatia demokrasia
Wakati huo huo Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amelaani mauaji ya Brahmi na kuushadidia wito uliotolewa na mkuu wa kitengo cha kutetea haki za binaadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay, shirika la Amnesty International na shirika la Human Rights Watch wa kutaka uchunguzi wa kina ufanyike juu ya mauaji hayo yaliolaaniwa pia na Marekani.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu