1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano nchini Venezuela

Maja Dreyer29 Mei 2007

Baada ya kufungwa kituo kimoja cha televisheni nchini Venezuela, maandamano dhidi ya hatua hii ya serikali yanaenea. Polisi jana ilitumia mabomba ya maji, mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya maelfu ya waandamanaji. Kituo cha RCTV kilijulikana kuipinga serikali ya rais Hugo Chavez.

https://p.dw.com/p/CB3u
Wanajeshi mbele ya kituo cha RCTV
Wanajeshi mbele ya kituo cha RCTVPicha: AP

Kituo cha televisheni cha RCTV ni kituo cha kwanza kabisa cha televisheni nchini Venezuela, lakini tangu usiku wa Jumatatu hakionekani tena. Serikali ya kisoshialisti chini ya rais Hugo Chavez ilikataa kurefusha leseni ya kituo hiki. RCTV ilituhumiwa kuliunga mkono kundi la wapinzani ambalo kwa mujibu wa serikali limepanga kuipindua serikali.

Wanafunzi kadhaa wa chuo kikuu walijeruhiwa kwenye maandamano yaliyotokea jana katika miji ya Caracas na Valencia. Mtangazaji mmoja maarufu wa RCTV alisema, kituo chake hakitanyamazishwa. Lakini tangu jana, bendi ya RCTV inatumika na kituo cha TEVES ambacho ni cha serikali. Wakati huo huo, wafuasi wa serikali walisherehekea kufungwa RCTV ambacho pamoja na upinzani wa kihafidhina na wa kiliberali kilikuwa kimekosoa vikali sera za rais Chaves.

Serikali pia ilipeleka ombi kwa ofisi ya uendeshaji mashtaka ya serikali kuchunguza kesi dhidi ya kituo kingine cha televisheni cha upinzani, Globovision. Shutumu ni kuwa, Globovision imetaka auliwe rais kwa kutumia taarifa za sirisiri. Mkuu wa Globovision, Alberto Federico Ravel, alikanusha tuhuma hiyo akiongeza kusema kwamba kituo chake hakitakubali kushindwa kutangaza kwa uhuru. Bw. Ravel: “Hatutabadilisha msimamo wetu kwamba hatuviogopi vitisho vya serikali hii, kwani ni kitu cha kawaida kuwa serikali ya kijeshi huwa haivipendi vyombo vya habari.”

Globovision sasa ni kituo kikubwa zaidi ambacho ni kwenye upande wa upinzani. Serikali inadhibiti viwili kati ya vituo vinne vya televisheni za taifa zima. Hatua ya serikali kukifunga kituo cha RCTV imezusha wasiwasi nchini Venezuela na nje. Gazeti moja kubwa limeandika huu ni mwisho wa kuwepo maoni tofauti nchini Venezuela. Askofu wa Merida, Venezuela, alimlinganisha Chaves na madikteta kama Hitler wa Ujerumani, Mussolini wa Italy au Fidel Castro wa Cuba.

Ujerumani kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya ilitaja wasiwasi wake juu ya kutokuwepo mashindano huru kutokana na kituo kilichofuata RCTV. Shirika linalotetea uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wasio na mipaka, limeilaumu hatua ya Venezuela kuwa inavunja uhuru wa kutoa maoni na kuathiri demokrasia.

Venezuela jana pia ilitoa shtaka dhidi ya kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, kwa kuwaunganisha rais Chaves na kundi la Al-Qaida katika matangazo yake. Waziri wa habari wa Venezuela, William Lara, alisema, picha za Chaves zilizoonyeshwa kwenye CNN ziliwekwa sambamba na picha za kiongozi mmoja wa al-Qaida. Juu ya hayo, CNN ililaumiwa kwa kutumia picha za Mexiko katika kuripoti juu ya maandamano nchini Venezuela.

Katika jibu lake, CNN ilikanusha kuhusishwa na kampeni dhidi ya serikali ya Venezuela. Kituo hiki kimekiri kuwa kimefanya kosa katika kuunganisha picha kutoka Mexiko katika taarifa juu ya Venezuela, lakini kwa bahati mbaya. Kuhusiana na al-Qaida, CNN ilisema katika kila kipindi taarifa mbali mbali tofauti huwa zinawekwa sambamba, kama katika ukarasa mmoja wa gazeti.