1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi yapanda taratibu Uhispania, Italia na Ujerumani

5 Aprili 2020

Kiwango cha maambukizi nchini Uhispania, Italia na Ujerumani kinaongezeka taratibu lakini mamia bado wanakufa kila siku. Wakati huohuo Marekani inaelekea katika kile kinachotarajiwa kuwa "wiki ngumu." 

https://p.dw.com/p/3aTtg
Spanien Corona-Pandemie
Picha: picture-alliance/dpa/E. Sanz

- Uhispania imeshuhudia siku nyingine ya kupungua kwa idadi ya vifo.

- Rais Donald Trump wa Marekani ameonya kuhusu "wiki ngumu" wakati taifa hilo likijiandaa kwa vifo vingi zaidi vya virusi vya corona

- Idadi ya visa vya maambukizi vinavyoripotiwa kila siku nchini Ujerumani imepungua kiasi, wakati taasisi ya Robert Koch ikiwa imerekodi visa chini ya 6,000.

Nchini Albania, visa vya virusi vya corona vimepanda kwa siku tatu mfululizo, huku mamlaka zikisema ongezeko hilo lilitokana na watu kutozingatia hatua za kujitenga. Taifa hilo la Balkani limeripoti visa vipya 28 hii leo. Hadi sasa, watu 361 wameathirika na virusi vya corona na 20 wamefariki dunia kwenye taifa hilo lenye watu milioni 2.68.

Huko Uingereza, kiongozi mpya wa chama cha Labour Keir Starmer ameituhumu serikali kwa kufanya "kosa kubwa" katika namna inavyolishughulikia janga hilo la corona. Kwenye habari iliyochapishwa na gazeti la Sunday Times, Starmer amesema mamlaka zimeshindwa kutoa visaa vya kutosha vya kujikinga kwa watoa huduma za afya na walikuwa nyuma katika hatua za vipimo. Aidha, ametoa mwito wa "programu ya kitaifa ya chanjo" dhidi ya virusi. Wizara ya afya imesema Jumapili hii kwamba idadi ya vifo nchini humo iliongezeka na kufikia 4,934 hadi jana baada ya kurekodiwa vifo vipya 621.

UK Neuer Labour Chef Keir Starmer
Keir Starmer amekosoa pakubwa namna serikali inavyoshughulikia mzozo wa virusi vya coronaPicha: picture-alliance/PA Wire/S. Rousseau

Maelfu ya wafungwa nchini Morocco wanatarajiwa kuachiwa huru ili kupunguza kitisho cha mripuko wa maradhi ya COVID-19 yanayoletwa na virusi vya corona, wizara ya sheria imesema leo Jumapili. Mfalme wa taifa hilo Mohammed VI ametoa msamaha kwa jumla ya wafungwa 5,654. Wafungwa walioachiwa walichaguliwa kwa kuzingatia umri, hali ya kiafya, muda waliotumikia kifungo na tabia zao wakati wakiwa gerezani. Taifa hilo la Afrika magharibi tayari limethibitisha visa 919 vya maambukizi na vifo 59. 

Rais wa Czechia, Milos Zeman amekosoa vikali namna Umoja wa Ulaya unavyokabiliana na janga hilo la virusi vya corona. "kwa bahati mbaya Umoja wa Ulaya umeshindwa katika suala hili," ameliambia gazeti la Blesk la nchini humo. Kiongozi huyo mwenye miaka 75, anayetambulika sana kwa matamshi yake makali, amemkosoa rais wa halmashauri ya Ulaya, Ursula von der Leyen, aliyepinga hatua ya kufunga mipaka ya Ulaya licha ya kutokuwa "mtaalamu".

Coronavirus Italien Varese Roboter hilft in Klinik
Italia inaandaa mpango wa kuirejesha nchi hiyo kwenye hali ya kawaida baada ya athari kubwa za coronaPicha: Reuters/F. Lo Scalzo

Serikali ya Italiacorona inajiandaa kupendekeza mpango wenye malengo matano unaolenga kufungua kwa hatua shughuli zilizositishwa nchini humo, waziri wa afya Roberto Speranza amesema. Italia ndio taifa lililoathirika zaidi na barani Ulaya. Alipozungumza na gazeti la Repubblica, Speranza amesema serikali itaendelea kutekeleza sheria ya kujitenga, kuboresha vifaa tiba vya kuwatibia watu wakiwa majumbani na kuongeza upimaji kwa kiasi kikubwa.

Soma Zaidi: Walioambukizwa COVID-19 wafikia zaidi ya laki tatu duniani

Sudan Kusini imeripoti kisa cha kwanza cha virusi vya corona. Nchi hiyo ni moja ya nchi za mwisho za Afrika kuthibitisha uwepo wa ugonjwa wa COVID 19 ndani ya mipaka yake. Akizungumza na waandishi habari mjini Juba makamu wa rais Riek Machar amesema mtu wa kwanza aliyeambukizwa virusi hivyo ni mwanamke aliye na miaka 29 aliyeingia Sudan Kusini akitokea Uholanzi kupitia Ethiopia tarehe 28 Februari. Uraia wake bado haujatajwa.

Taarifa kutoka kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS zinasema mwanamke huyo ni mtumishi wao. Machar amesema Wizara ya afya kwa kushirikiana na shirika la afya duniani WHO na shirika la kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kuwafuatilia wote walioikaribiana na mwanamke huyo.

Ethiopia nayo imethibitisha kifo cha kwanza cha COVID-19. Aliyefariki ni mwanamke wa miaka 60 aliyekuwa akipatiwa matibabu hospitalini mjini Addis Ababa tangu Machi 31, waziri wa afya Lia Tadesse amesema leo Jumapili. Taifa hilo la upmbe wa Afrika lina visa 43 vya maambukizi na limeripoti watu wanne tayari wamepona maambukizi hayo ya virusi vya corona.

Mashirika.