1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya corona duniani yapindukia milioni 5

21 Mei 2020

Zaidi ya watu milioni tano wameambukizwa virusi vya corona duniani na zaidi ya 327,000 wamefariki, wakati ambapo Shirika la Afya Duniani, WHO limeripoti ongezeko kubwa zaidi la maambukizi ya corona kwa siku moja.

https://p.dw.com/p/3ca0o
Schweiz Genf WHO Treffen | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: picture-alliance/Xinhua/WHO

Shirika la Afya Duniani limesema kuwa zaidi ya maambukizi 106,000 yameripotiwa kwa siku moja jana, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kwa siku tangu mripuko wa virusi vya corona katika mji wa Wuhan huko China mwezi Desemba. Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali katika mataifa masikini duniani.

Bara la Ulaya linaonekana kuwa limevuka kilele cha maambukizi huku idadi ya visa vipya na vifo ikionekana kushuka kila siku jambo linalotoa nafasi kwa baadhi ya nchi kulegeza vikwazo vyake.

Urusi Jumatano ilirekodi kiasi kidogo zaidi cha maambukizi tangu Mei mosi huku wagonjwa wengi wakiruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani. Kulingana na maafisa nchini Urusi, hii inaonyesha kwamba maambukizi hayaongezeki tena kwa sasa.

Marekani inaendelea kuilaumu China kuhusiana na Corona

Nchini Italia viwanja vya ndege vimeruhusiwa kufunguliwa tena kuanzia Juni 3 ambapo ndege za kimataifa pia zitaingia nchini humo.

Na Marekani, nchi ambayo imeathirika zaidi duniani, maafisa wa serikali wanaendelea kuilaumu China kwa jinsi ilivyoshughulikia mripuko wa virusi vya corona. Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo amedola bilioni mbili zilizoahidiwa na China katika kupambana na janga hili ni fedha kidogo mno, ikilinganishwa na mamia kwa maelfu ya watu walioaga dunia na hasara ya matrilioni ya pesa.

Symbolbild Mike Pompeo in Afghanistan
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike PompeoPicha: imago images/Xinhua/L. Jie

Huko Amerika ya Kusini nako, hali imezidi kuwa mbaya zaidi nchini Brazil na taifa hilo huenda likawa la pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi. Nchi hiyo ilitoa mwongozo kwa raia wake kutumia dawa ya kutibu malaria Hydroxychloroquin katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Mayra Pinheiro ni afisa katika wizara ya afya Brazil.

"Daktari ndiye anayeamua kumpa mgonjwa dawa hiyo, na mgonjwa ana haki ya kuikubali au kuikataa. Tunawafahamisha kabisa kuhusiana na athari zake," alisema Mayra Pinheiro.

Afrika Kusini yaripoti kifo cha kwanza cha mtoto mchanga kutokana na Corona

Barani Asia nako maambukizi nchini Japan yanapungua na nchi hiyo italegeza baadhi ya vikwazo katika miji ya Osaka, Kyoto na Hyogo Alhamis.

Japan Ministerpräsident Shinzo Abe
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Imago Images/Kyodo

Thailand imesema inatarajia chanjo ya virusi vya corona iwe tayari mwakani, baada ya majaribio yaliyofanyiwa panya kuonyesha matumaini.

Barani Afrika, Wizara ya afya Afrika Kusini imeripoti kifo chake cha kwanza kinachohusiana na corona kwa mtoto mchanga wakati ambapo idadi ya vifo nchini humo imefikia watu 339.

Huku idadi ya maambukizi na wanaofariki ikiongezeka kote duniani kila uchao, serikali zinataraji kwamba chanjo itapatikana hivi karibuniili ziweze kuzinusuru chumi ambazo zimeathirika vibaya. Ila kulikuwa na habari ya kutia moyo Jumatano, kwani tafiti zilizofanyiwa tumbili zilionyesha kwamba binadamu wanaweza kupata kinga dhidi ya virusi vya corona.