1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Loew: Hakujawahi kuwa na ubaguzi katika timu ya taifa

Sekione Kitojo
29 Agosti 2018

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew amekiri kufanya makosa kadhaa ambayo yalichangia katika hali mbaya iliyojitokeza katika kombe la  dunia lakini ameamua kuchukua hatua chache za kufanya mabadiliko katika kikosi chake.

https://p.dw.com/p/33y4m
Deutschland Präsentation der Analyse zur Fußball-WM | Joachim Löw und Oliver Bierhoff
Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Amefanyia  mabadiliko  kikosi kitakachoshiriki katika michezo ya  kimataifa mwezi  ujao, akisema, mlingano  wa  kuwa  na uzoefu pamoja  na  vijana ni  muhimu. Loew  alisema  leo (29.08.2018) kwamba  Ujerumani, ambayo ilitolewa  mapema katika  kombe  la  dunia  kwa  mara  ya  kwanza  katika  muda  wa  miaka  80 katika awamu ya  makundi,  haikupaswa  kucheza mchezo  wao  wa kawaida  wa kumiliki  mchezo  katika  mashindano  hayo  ya  mtoano wakati  timu  zilikuwa  zikifanya mashambulizi  ya  ghafla  kwa  mafanikio  makubwa.

Deutschland Präsentation der Analyse zur Fußball-WM | Joachim Löw
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim LoewPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Pia  amesema  alishindwa  kuingiza  hali  ya kuona  umuhimu  na  hisia  miongoni  mwa wachezaji  wake  ambao  walipoteza  michezo  yao  miwili  kati  ya  mitatu  katika  awamu ya makundi.

Miongoni mwa  wachezaji  aliowaita  katika  kikosi  cha  Ujerumani  katika  michezo  ya  ligi ya  mataifa  dhidi  ya  Ufaransa  Septemba  6  na   mchezo  wa  kirafiki  dhidi  ya  Peru  siku tatu  baadaye, ni  wachezaji  wanaorejea  katika  kikosi  hicho Leroy Sane, Nils  Petersen  na jonathan Tah  pamoja  na  wageni  Kai Havertz, ambaye  ana  umri  wa  miaka  19 , Thilo Kehrer , mwenye  umri  wa  miaka  21, na Nico Shulz  mwenye  umri  wa  miaka  25.

Schweiz gegen Deutschkand - Freundschaftsspiel
Mchezaji bora kijana katika ligi ya England Leroy Sane amerejea katika kikosi cha timu ya taifaPicha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

"Uzoefu ni  msingi  muhimu  hata  kwa wanaoanza  upya," Loew alisema. "Na  wachezaji vijana, wenye  uchu  wanaweza  kusaidia  katika  majukumu  muhimu  siku za usoni."

Mchezaji bora  wa  Premier League

Mshambuliaji  wa  pembeni Sane, ambaye  alichaguliwa  kuwa  mchezaji  bora kijana  katika ligi  ya  England  ya  Premier League msimu  uliopita  baada  ya  kuisaidia  Manchester  City kupata  ubingwa, Petersen na  Tah  waliondolewa  kutoka  katika  kikosi  cha  mwisho kilichoshiriki  katika  fainali  za  kombe  la  dunia  nchini  Urusi  mwezi  Juni.

Loew amemuacha  mchezaji  wa  kati Sami Khedira, aliyekuwamo  katika  kikosi kilichoshinda  kombe  la  dunia mwaka  2014, kwa  ajili  ya  mechi za  mwezi  ujao lakini ameendelea  kuwa  na  imani  na  wengine  kadhaa  ambao  wamecheza  chini  ya  kiwango nchini  Urusi,  miongoni  mwa  wachezaji  17  kati  ya  23  waliokuwa  katika  kikosi kilichokwenda Urusi.

"Umiliki  wa  mpira  katika  ligi ni  muhimu  lakini  katika  awamu  ya  mtoano  kunahaja  ya kubadilika. Hilo  lilikuwa  kosa  langu  kubwa," Loew  aliwaambia  waandishi  habari. "Kwamba  naamini kwa  mchezo  wa  kumiliki  mpira  tutapita  katika  awamu  ya  makundi.

Testspiel Deutschland Saudi Arabien Sami Khedira
Mchezaji wa kati wa Ujerumani Sami KhediraPicha: picture alliance/augenklick/firo Sportphoto

"Nilitaka  kufanya  bora  zaidi, na kufanya bora  zaidi umiliki  wa  mchezo . Lakini  kila mchezo  ni  wa  mtoano. Nilipaswa  kutambua kwamba  tunahitaji  kuchukua tahadhari  zaidi. Badala  yake  nilitaka  kuingia  katika  hatari zaidi."

Loew  pia  amesema  alishindwa  kuwatia  hamasa  zaidi  wachezaji  wake  kwa  ajili  ya michuano  hiyo.

"Baada  ya  kushinda  mwaka 2014 na  kuwa  juu tulishindwa  mara  hii , kuwasha  moto mkubwa  ili kila  mmoja  ajihisi kuwa  na  hamasa," Loew  alisema.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Idd Ssessanga