1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Libya yawahukumu kifo wanachama 17 wa IS

20 Desemba 2022

Mahakama ya Libya imewahukumu adhabu ya kifo watu 17 baada ya kukutwa na hatia ya kujiunga na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na kufanya mashambulizi kwa kutumia jina hilo.

https://p.dw.com/p/4LDH7
Mutmaßliche Taliban-Mitglieder bei verschiedenen Operationen festgenommen
Picha: Ghulamullah Habibi/epa/picture alliance/dpa

Mwendesha mashtaka alisema jana kuwa mahakama ya Tripoli pia imewahukumu watu wawili kifungo cha maisha gerezani na wengine 14 vifungo vidogo jela.

Taarifa ya mwendesha mashtaka imeeleza kuwa watu hao walikutwa na hatia ya kufanya shughuli zinazohusishwa na IS, pamoja na ghasia za kutumia silaha kwenye mji wa Sabratha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu walioshtakiwa wamewaua jumla ya watu 53 na kuharibu majengo ya umma. Uraia wa watu waliohukumiwa kifo haujatangazwa.

Mwaka 2010, Libya ilipiga kura kupinga azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa kwa adhabu ya kifo duniani kote, lakini haijachapisha takwimu za kuaminika kuhusu adhabu ngapi kama hizo ambazo zimetolewa.