1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yakabiliwa na kitisho cha kuporomoka kwa uchumi

27 Agosti 2024

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umetoa taarifa ukieleza wasiwasi wake juu ya kile walichokitaja kama "hali inayozidi kuzorota nchini humo na ambayo imetokana na maamuzi ya upande mmoja.”

https://p.dw.com/p/4jwlG
Stephanie Williams, Kaimu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Libya UNSMIL.
Stephanie Williams, Kaimu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Libya UNSMIL.Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Migogoro kuhusu usimamizi wa benki kuu ya Libya imezua hofu kuhusu uwezekano wa matumizi mabaya ya raslimali za kifedha nchini humo.

Taarifa ya UNSMIL imeeleza kuwa, ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umeitisha mkutano wa dharura na pande zote zinazohusika katika mgogoro juu ya usimamizi wa benki kuu ya Libya ili kufikia makubaliano yatakayozingatia maelewano ya kisiasa, sheria zinazotumika na kanuni ya uhuru wa benki kuu.

Soma pia: Benki Kuu ya Libya yasitisha shughuli zake

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa kusitishwa kwa maamuzi ya upande mmoja, kuondolewa kwa hali ya dharura katika visima vya mafuta, kusitishwa kwa mivutano na hakikisho la ulinzi wa wafanyikazi wote wa benki kuu.

Uchumi wa Libya unategemea kwa kiasi kikubwa mapato yanayotokana na uuzaji wa mafuta.

Hata hivyo kumewekwa hali ya dharura katika visima vya mafuta, na hivyo kukatisha chanzo kikuu cha mapato ya nchi hiyo.

Mapema jana Jumatatu, utawala wa Libya upande wa mashariki uliamuru kufungwa kwa visima vya mafuta mashariki mwa nchi hiyo, hatua iliyositisha uzalishaji na usafirishaji wa mafuta baada ya kuibuka kwa mivutano kuhusu usimamizi wa benki kuu.