1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon katika mzozo wa kisiasa

Miraji Othman22 Novemba 2007

Lebanon inasheherekea leo maadhimisho ya mwaka wa 64 wa uhuru, lakini nchi hiyo inakabiliwa na mzozo mkubwa kabisa wa kisiasa. Kama itaweza kuibuka salama, itajulikana baada ya kesho.

https://p.dw.com/p/CRu4
Rais mstaafu wa Lebanon, Emile Lahoud.Picha: AP

Wananchi wa Lebanon leo wanaadhimisha mwaka wa 64 wa uhuru wa nchi yao, huku wakiwa katika hali ya wasiwasi mkubwa kuhusu mustakbali wa kisiasa wa nchi yao. Viongozi wa nchi hiyo wanaogombana bado hadi dakika hii hawajakubaliana juu ya mtetezi atakayekubalika kuwania wadhifa wa rais wa nchi hiyo. Bunge linatakiwa likutane kesho saa saba za mchana kuchagua mtu atakayekamata nafasi ya rais wa sasa, Emile Lahoud, ikiwa ni saa 11 tu kabla ya kipindi cha rais huyo kumalizika.

Sio tuu wanasiasa wa nchi hiyo walioko mbioni kutafuta muwafaka wa dakika ya mwisho kuinusuru nchi yao isitumbukie katika janga lisilojulikana, lakini pia mataifa makuu ya nje yanashiriki kutafuta mtu atakayekubalika na pande zote za kisiasa katika nchi hiyo kuwa rais. Wananchi wengi wa Lebanon wanasema wana wasiwasi kama wanasiasa wao wataweza kuzuwia ushawishi wa kigeni katika suala hilo. Na hapo linazuka suala linalofaa sana kujibiwa siku kama ya leo ya kuadhimisha uhuru wa Lebanon. Jee kweli nchi hiyo ni huru?

Katika umbo lake la sasa, Lebanon ilianza kupewa sura na Wafaransa hapo mwaka 1920, na katika historia yake ya misukosuko, zaidi ya dazeni za serekali za kigeni ziliwahi kutuma majeshi katika nchi hiyo, mara nyingi kwa kibali na mara nyingine bila ya kibali cha serekali zenyewe za Lebanon. Israel iliivamia nchi hiyo mara tatu, majeshi ya Marekani yalijiingiza mara mbili kuziunga mkono serekali ilizozitaka na majeshi ya Syria yalibakia huko tangu mwaka 1976 hadi yalipoondoka mwaka 2005 kwa amri ya Umoja wa Mataifa. Nchi nyingine zimechangia katika jeshi la amani la Umoja wa Mataifa lililowekwa katika mpaka na Israel tangu mwaka 1978.

Ikiwa ni nchi ndogo katikati baina ya majirani wenye nguvu, tena mahasimu, Israel na Syria, katika miongo minne iliopita Libanon imegeuzwa kuwa ni uwanja wa malumbano pale moja katika ya mahasimu hao wawili anapotaka kuyagonga maslahi ya upande mwengine.

Ilivokuwa sasa ni masaa machache kabla ya kumalizika kipindi cha Rais Emile Lahoud, na hakuna muwafaka hadi sasa juu ya nani atachukuwa mahala pake, ushawishi wa kigeni unaonekana wazi wazi ukizidisha misuli juu ya nani atakalia kiti cha urais. Syria iko nyuma ya muungano wa upinzani unaoongozwa na Chama cha Washia cha Hizbullah. Na kwa upande mwengine, Marekani, ikiuungwa mkono na Ufaransa na Saudi Arabia, inashikilia kuweko mtetezi atakayefaa kwa maslahi yake. Picha ya katuni katika gazeti moja la Beirut imedhihirisha ile hisia iliotanda. Kuna picha ya bendera ya Lebanon, nusu moja ya bendera hiyo iko vile vile, lakini nusu ya pili imesheheni bendera za Misri, Syria, Iran, Russia, Ufaransa na Marekani, huku kiti cha rais kikiwa kitupu baina ya bendera hizo.

Zoezi la kumchagua rais lililokuwa limepangwa Septemba 25 mwaka huu, limeahirishwa mara nne. Kuna dalili kwamba kikao cha kesho hakitafanyika. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa na Spain wamekuwa wakienda huku na kule, baina ya pande mbili za wanasaiasa wa Lebanon, kutafuta suluhu , lakini bila ya mafanikio. Jeshi na polisi zilizidisha ulinzi katika mji mkuu wa Beirut, na hakujakuweko paredi ya kuadhimisha leo siku ya uhuru. Upinzani unaoongozwa na Chama cha Hizbullah umesema hautakwenda bungeni kabla ya kwanza kufikiwa makubaliano juu ya mtetezi wa urais, ambaye kazima awe Mkristo wa madhehebu ya Maronite, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo inayogawa madaraka kwa mujibu wa madehehbu ya kidini. Pindi hakutachaguliwa rais, basi rais wa sasa, Emile Lahoud, amesema atachukuwa hatua za kuhakikisha umoja wa nchi hiyo unabakia. Hiyo inaweza kuwa ni kukabidhi madaraka kwa jeshi kuliko kumwachia waziri mkuu wa sasa, Fouad Siniora. Lahoud na upande wa upinzani wanasema serekali ya Siniora imepoteza uhalali wake pale mawaziri wote wa Kishia walipojiuzulu mwaka jana. Kushindwa kuchaguliwa rais kabla ya kesho saa saba za mchana kutasababisha kuweko pengo, au hata kuweko serekali mbili zinazopingana, kama vile ilivokuwa katika miaka mwili ya mwisho ya vita vya kienyeji vya mwaka 1975 hadi 1990. Tuombe tuu kutokee muujiza.