1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufuatia kupanda bei ya mchele, bara la Asia kukabiliwa na njaa.

Scholastica Mazula21 Aprili 2008

Ongezeko la bei za vyakula katika nchi mbalimbali barani Asia limeendelea kuwa kubwa zaidi.

https://p.dw.com/p/Dlps
Muuzaji wa mchele katika ghala la Serikali akiuza nafaka hiyo mjini Nawabganj , Dhaka, nchini Bangladesh, April 11, 2008.Picha: AP

Hali hii imesababisha Serikali za nchi hizo kuingilia kati na kudhibiti bei za mchele kwa kuhofia upungufu wa zao hilo hapo baadaye na kuleta mgogoro wa chakula kwa jamii.

Hali ya kuongezeka bei ya mchele Barani Asia kila kukicha inazidi kuwarejesha raia wake nyuma kimaendeleo na kuzidi kuwadidimiza katika Umasikini.

Akizungumzia Tatizo la upungufu wa chakula duniani katika ufunguzi wa Mkutano wa Shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-Moon, alisema tatizo la njaa halikusabishwa na kupanda kwa bei za vyakula pekee bali pia mabadiliko ya hali ya hewa na mafuta kupanda.

Katika mahojiano maalumu na Shirika la habari la IPS, Msemaji wa Shirika la Mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, Barani Asia-WFP, Paul Risely, amesema ungezeko la bei za vyakula katika bara hilo linachukuliwa kama kitendo cha kurejesha nyuma bahati ya uchumi mzuri uliokuwepo kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Bei ya Mchele ambao ndilo zao kuu katika bara hilo, imekuwa ikiongezeka kila wiki sasa tangu kuanza kwa mwaka huu.

Katika baadhi ya maeneo kama ya Kusini Mashariki mwa Asia, kiwango cha ununuzi wa mchele kimekuwa kikubwa zaidi na kuhofiwa kuwa huenda ikazidisha upungufu ama kumalizika kabisa kwa zao hilo katika maghala na masoko ya chakula.

Mashirika ya misaada ambayo yamekuwa yakifanya kazi miongoni mwa watu masikini, likiwemo WFP,yanahofia kwamba endapo hali hii itaendelea, hivi karibu watasitisha utoaji wa miasaada yao ya chakula.

Mtaalamu wa masuala ya chakula kutoka Shirika la ActionAid, John Samuel, ameiambia IPS, kuwa tatizo hilo litaongeza ukosefu wa chakula katika maeneo ya watu masikini zaidi barani Asaia.

Kwa mujibu wa WFP, tayari idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula imeongezeka. Nepal, idadi ya watu milioni nane wako katika hatari ya kukabiliwa na njaa endapo bei za vyakula zitaendelea kupanda.

Nchini Bangladesh, kwa zaidi ya wiki mbili sasa zilizoopita, kumekuwako misururu mirefu ya watu kila siku katika maghala ya vyakula ya Serikali wakisubiri kununua mchele na bidhaa nyingine.

Hali ni ileile pia katika nchi za philipines, Pakistan,China na Indonesia, ambako kumekuwa na hofu kubwa juu ya ukosefu wa chakula naa njaa kutokana na kupanda kwa bei za vyakula katika soko la dunia.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba tatizo hili la chakula lilikuwa likingojewa kutokea kwa sababu ulaji wa mchele umekuwa mkubwa zaidi kuliko uzalishaji wa zao hilo katika kipindi cha miaka kumi.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, suluhisho pekee la hali iliyopo kwa sasa ni uwekezaji mkubwa katika kilimo.