1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuchaguliwa Papa na miaka 10 ya Ajenda 2010

13 Machi 2013

Mbali na zoezi la kumchagua kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,wahariri wamejishughulisha pia na masuala ya familia na miaka 10 ya ajenda 2010

https://p.dw.com/p/17vyu
Waumini wamekusanyika katika uwanja wa Petrus mjini Roma wakisubiri kuona moshi mweupePicha: Reuters

Tuanzie lakini Roma na zoezi la kumchagua kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni baada ya moshi mweusi kufuka katika paa la kanisa ndogo la Sistin magharibi ya jana. Makadinali 115 wanaendelea na zoezi hilo hii leo. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:

Kanisa linahitaji kiongozi atakayeleta mageuzi, anayeelewa kwa nini watu wengi barani Ulaya wanalipa kisogo kanisa - kiongozi anayeweza kutambua mahitaji watu walio nayo wakati huu. Lakini ikiwa kweli mtu kama huyo ana nafasi ya kuchaguliwa, hakuna ajuaye. Pengine mzozo umezidi makali kutokana na kujiuzulu Benedikt wa 16 kwa namna ambayo makadinali wanaona bora wampate mpenda mageuzi. La kama sivyo, basi kanisa litakuwa linapotelewa na wakati, hali ya kuaminika na kuwapoteza pia wengi wa waumini wake.

Familia zenye watoto zinakabiliana na changamoto kubwa ikiwa baba na mama wanafanya kazi. Vipi kuirahisishia maisha familia ni suala lililojibiwa na gazeti la "Hannoversche Allgemeine" .

Familia na jukumu la kazi na kulea watoto

Deutschland Familiengipfel 2013 in Berlin Familienministerin Kristina Schröder
Waziri wa familia Kristina Schröder(kushoto) na kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/BREUEL-BILD

Haki ya kurejea kikamilifu kazini baada ya kufanya kazi nusu nusu, inaweza kuzisaidia familia nyingi.Lakini kimsingi ni jukumu la makampuni kutambua kwamba ufanisi wa kiuchumi utategemea jinsi mama na baba wanavyokidhiwa mahitaji yao, yanayoanzia na kuwepo vituo vya chekechea katika mahala wanakofanya kazi, ili kuwatunza watoto wao hadi kufikia muda maalum wa kufanya kazi. Hili ni suala la mageuzi katika desturi za kufanya kazi.

Maoni sawa na hayo yametajwa pia na gazeti la "Nordkurier" linaloendelea kuandika:

Kupanga muda wa kufanya kazi unaolingana na ratiba ya familia, kuruhusiwa familia zifanye kazi kwa muda tu, na kufunguliwa vituo vya kuwahudumiwa watoto wadogo kazini - hayo ndio matamshi yaliyotolewa na Kansela Angela Merkel na waziri wa masuala ya familia, Kristina Schröder. Ni matamshi mazuri mtu akiyasikia -La ziada hakuna. Ni maneno matupu ambayo ni vigumu mno kuyatekeleza.

SPD na ajenda 2010

10 Jahre Agenda 2010 Schröder Archivbild 2003
Kansela wa zamani Gerhard Schröder akitetea Ajenda 2010 mnamo mwaka 2003.Picha: picture-alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kuadhimishwa miaka kumi tangu mkakati wa kuhimiza nafasi za kazi na kuwapa moyo wasiokuwa na ajira wawajibike zaidi ulipoanza kutumika.Kifungu kimojawapo kinahusiana na malipo ya wasiokuwa na ajira mashuhuri kwa jina Hertz nambari 4. Muasisi wa mkakati huo alikuwa kansela wa zamani Gerhard Schröder kutoka chama cha Social Democratic - SPD. Gazeti "Cellesche Zeitung" linaandika:

SPD hawawezi kushinda uchaguzi kutokana na mkakati wa Hertz nambari nne. Hata mwaka huu wa 2013 hawatoweza. Ndio maana mpango mpya ulioandaliwa na wana Social Democratic, unazungumzia kuhusu kiwango cha chini cha mishahara, kuongezwa kiwango cha kodi za mapato na kuzidishwa huduma za jamii. Hilo halijalengwa pekee kumaliza mfarakano pamoja na wafuasi wa mrengo wa shoto ndani ya chama cha SPD, uliosababishwa na mkakati wa Ajenda 2010, bali pia kuwavutia wapigakura wa chama cha mrengo wa shoto die Linke - Na hilo linaweza kufanikiwa.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef