1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korti yasema kesi ya ugaidi ya Mbowe kuendelea

1 Septemba 2021

Jaji mmoja wa mahakama kuu mjini Dar es Salaam Elinaza Luvanda amesema leo kuwa kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe inaweza kuendelea.

https://p.dw.com/p/3zlS2
Tansania | Prozess gegen Chadema Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Jaji mmoja wa mahakama kuu mjini Dar es Salaam  Elinaza Luvanda amesema leo kuwa kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe inaweza kuendelea.

Jaji Luvanda ametupilia mbali pingamizi zilizokuwa zimewasilishwa na chama chake cha Chadema.

Kusikilizwa kwa pingamizi hizo kumefanyika chini ya ulinzi mkali huku baadhi ya wawakilishi kutoka balozi za kigeni na viongozi waandamizi wa Chadema wakihudhuria lakini waandishi wengi wa habari wamenyimwa fursa ya kuingia mahakamani na polisi.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema pamoja na wafuasi wake wanasema mashtaka hayo yamechochewa kisiasa na ni juhudi za kukandamiza upinzani na wamewatuhumu polisi kwa kumtesa akiwa kizuizini.

Mbowe mwenye miaka 59 amezuiliwa na polisi tangu Julai 21 alipokamatwa pamoja na maafisa wengine wa Chadema saa chache kabla kufanya mkutano wa hadhara kushinikiza mabadiliko ya katiba.