1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korti Kenya zasitisha huduma kumuomboleza hakimu aliyeuawa

18 Juni 2024

Idara ya mahakama nchini Kenya imesitisha huduma zake kwa leo ili kumuomboleza Hakimu mkuu Monica Kivuti aliyeuawa akiwa kazini kwenye mahakama ya Makadara Alhamisi iliyopita.

https://p.dw.com/p/4hBoi
Kenia Wahlen 2022
Picha: John Ochieng/SOPA Images/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Bendera ya idara hiyo inapepea nusu mlingoti hadi marehemu atakapozikwa. Mahakimu na majaji wanaandamana kwa amani kupinga ukosefu wa usalama kwenye sehemu zao za kazi.

Maafisa wa ngazi ya juu walikusanyika kwenye mahakama ya Milimani jijini Nairobi kumuenzi na kumuomboleza hakimu mkuu Monica Kivuti aliyeuawa Alhamisi iliyopita. Maombolezi ya leo yanaongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Hakimu Monica Kivuti alipigwa Risasi alipokuwa kazini kwenye mahakama ya Makadara na afisa wa ngazi ya juu wa polisi. Afisa huyo wa polisi, inspekta Samson Kipchirchir Kipruto aliyesimamia kituo kimoja cha polisi huko Londiani, kaunti ya Kisumu naye aliuawa kwenye purukushani hizo.

Polisi huyo aligadhabika baada ya Hakimu Kivuti kufutilia mbali dhamana aliyopewa mkewe ambaye anaandamwa na mashtaka ya kujipatia hela kinyume na sheria. Mshtakiwa huyo anayedai kuugua alikosa kufika mahakamani Mara kadhaa Jambo lililomsukuma Hakimu Kivuti kufutilia mbali dhamana na kuamuru azuiliwe kwenye jela ya Langata ya wanawake.

​​​​Jaji Mkuu Martha Koome amebainisha kuwa huduma zitarejeshwa kuanzia Jumatano.
​​​​Jaji Mkuu Martha Koome amebainisha kuwa huduma zitarejeshwa kuanzia Jumatano.Picha: John Ochieng/SOPA Images/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Kufuatia tukio hilo, idara ya mahakama sasa imesitisha kusikiliza kesi nje, kwenye nyumba za Mabati au popote pasipokuwa sehemu rasmi ya majengo ya mahakama ili kulinda usalama wao. Hayo yametangazwa na Jaji Mkuu Martha Koome na kuungwa mkono na naibu Rais wa chama cha majaji na mahakimu KMJA, Zachary Kiongozi.

Ifahamike kuwa mahakama kote nchini zimefungwa Jumanne kwa heshima ya marehemu Hakimu mkuu Monica Kivuti wa mahakama ya Makadara.

Rais Ruto alaani kitendo cha polisi kumpiga hakimu risasi

Rais William Ruto aliyerejea nchini mwanzoni mwa Wiki kutokea Italia na Uswisi amekashifu mauaji hayo na kuitaka idara ya polisi kuimarisha ulinzi mahakamani.

Marehemu Hakimu Monica Kivuti ameacha watoto watatu, wa mwisho ni mchanga wa miezi 18. Atazikwa kwao Yatta.

Itakumbukwa kuwa mwaka 1999, Hakimu Mkuu wa mahakama ya Nakuru Babu Achieng akiandamana na mwanawe Neremy alipigwa risasi hadi kufa akiwa madukani wakati wa jioni mtaani Kilimani.