1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatoa onyo.

Halima Nyanza8 Aprili 2009

Saa kadhaa baada ya Korea Kaskazini kutoa picha zinazoonyesha ushindi kwa kile ilichokiita sehemu ya mradi wake wa amani wa anga za juu, imeonya kuchukua hatua kali iwapo Umoja wa Mataifa utachunguza hatua ya nchi hiyo

https://p.dw.com/p/HSTj
Wakorea kusini wakitazama habari katika TV, juu ya Korea Kaskazini kurusha rocket yake.Picha: AP

Marekani na Washirika wake wamekuwa wakilishinikiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua kali nchi hiyo, kwa kile wanachokiona kama ni jaribio la kichokozi la kombora lake la masafa marefu na kukaidi maazimio yaliyopita ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yanakataza nchi hiyo kurusha kombora lenye masafa, hatua ambayo ilichukuliwa baada ya Korea kaskazini kufanya jaribio lake la nyuklia mwaka 2006 na mazoezi mengine ya makombora.


Lakini Marekani na washirika wake ikiwemo Japan, imekuwa ikipata upinzani kutoka China, Urusi na mataifa mengine.


Naibu Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa Pak Tok Hun amesema iwapo wanachama 15 wa baraza hilo wataichukulia nchi hiyo hatua yoyote watazingatia hilo, kuwa ni kuingilia mipaka ya nchi yao, hivyo hatua ijayo itakuwa ni zamu yao kuchagua.


Amesisitiza kuwa kila nchi ina haki ya kutumia uwanda wa juu kwa amani na kutolea mfano kwamba nchi nyingi tayari zimerusha satelite zao angani na kwa mara kadhaa.


Ameongeza kusema kuwa kama ili kuwa sawa kwa nchi hizo kurusha satelite zao, kwanini wao wanakatazwa kufanya hivyo, basi hiyo siyo haki.


Naibu Balozi huyo wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa roketi iliyorushwa siku ya Jumapili ilikuwa ni roketi na sio kombora na kwamba kila mtu anaweza kutofautisha kati ya kombora na roketi.


Tayari Korea Kaskazini imeonya kujitoa katika mazungumzo ya pande sita, yanayofanywa katika juhudi za kutaka nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kuzalisha nyuklia, iwapo itachukuliwa hatua yoyote na Umoja wa Mataifa.


Awali China ilisema kuwa Pyongyang ina haki ya kutumia anga kwa amani.


Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema mataifa yenye nguvu yanapaswa kujizuia na uamuzi wa hamaki dhidi ya Korea kaskazini.


Wakati Korea Kaskazini ikisisitiza kuwa Satelite yake imefika katika katika mzunguuko wa Orbit, Korea Kusini, Japan na Marekani zinasema hakuna dalili zozote ya Satelite iliyofika huko.


Korea Kaskazini imesema roketi hiyo iliyobeba satelite ya mawasiliano, hata hivyo Marekani na washirika wake wanasema zoezo hilo ni la kujaribu kombora lake la masafa marefu ambalo likirushwa linaweza kufika Alaska au Hawaii.


Katika hatua nyingine Japan imesema picha iliyotolewa na Korea Kaskazini ikionesha roketi hiyo ikiruka siku ya Jumapili, inaonesha maendeleo ya teknolojia iliyopata nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni.


Katibu wa Baraza la Mawaziri nchini Japan Takeo Kawamura amesema filamu hiyo imeonesha kuwa roketi hiyo ilivyorushwa kulikuwa na maendeleo zaidi kushinda awali na kwamba ilikuwa kubwa kushinda nyingine zilizowahi kurushwa na Korea Kaskazini.


Pyongyang iliwahi kurusha kwa majaribio roketi yake mwaka 2006, lakini ililipuka baada ya sekunde 40 na kwamba mwaka 1998 ilirusha kombora lake la masafa mafupi, ikiwa ni sehemu ya kushindwa kurusha satelite yake.


Mwandishi: halima Nyanza /AFPE

Mhariri.M.Abdul-Rahman