Kony ashindwa kufika katika utiaji saini.
1 Aprili 2008Kampala.
Kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army , Joseph Kony, ameahirisha utiaji saini makubaliano ya amani kutokana na kuugua.
kony alikuwa atie saini makubaliano ya mwisho ya amani na serikali ya Uganda siku ya Alhamis.
Maendeleo katika mazungumzo hayo ya amani yanayofanyika katika nchi jirani kusini mwa Sudan baada ya karibu mwezi mzima wa mkwamo , yamezusha matumaini ya kumalzika kwa miongo miwili ya mzozo huo ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha karibu watu milioni mbili kuyakimbia makaazi yao.
Waganda wengi wamebaki na shaka iwapo Kony atatia saini makubaliano hayo ya mwisho ya amani na baadhi ya maafisa wa serikali wamekishutumu kikundi cha LRA kwa kutumia mazungumzo hayo kupoteza muda tu na kulipatia jeshi lao silaha mpya.
Kony pamoja na wasaidizi wake wawili wanatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague kwa makosa kadha ya uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na kuwakamata watoto.