KOMBE LA MASHIRIKISHO:MEXICO 1 BRAZIL 0-KOMBE LA DUNIA KANDA YA AFRIKA
20 Juni 2005Leo ni mapumziko katika Confederations Cup-kombe la mashirikisho hapa Ujerumani ambalo linafungua pazia la Kombe la dunia mwakani nchini Ujerumani.
Mexico itakayokutana ama na Ujerumani au Argentina katika nusu-finali ya Confederations cup inaamini itatawazwa tena mabingwa wa Kombe hili.Hii ni baada ya kuichapa Brazil jana bao 1:0.bao la jared Borsetti la kichwa katika kipindi cha pili lilitosha kuipatia Mexico tiketi ya nusu-finali na kuiacha Brazil kutapatapa sasa ikisubiri matokeo kati yake na Japan ilioilaza jana Ugiriki mabingwa wa Ulaya kwa bao 1:0.
Kocha wa Mexico Ricardo la Volpe ameiongoza Mexico kushinda mara 19 tangu kushindwa na Brazil Julai mwaka jana katika Copa America.Mexico ilitwaa Kombe hili 1999 ilipoilaza Brazil 4-3 mjini Mexico city.Ushindi wa jana wa Mexico umekuwa wa 7 katika mechi 33 kati yao.
Brazil ina miadi na japan jumatano hii mjini Cologne kujua hatima yake katika Kombe hili.Masashi Oguro aliipatia Japan bao dakika 14 kabla ya firimbi ya mwisho na kuwapiga kumbo mabingwa wa ulaya Ugiriki mjini Frankfurt jana.Sasa hatima ya Brazil itaamuliwa na Mbrazil, Zico kocha wa Japan.
Jumamosi, mabingwa mara 3 wa dunia na wenyeji Ujerumani walitokwa na jasho hadi dakika 16 za mwisho walipofaulu kupöitia mkwaju wa penalty kuzima ubichi wa mabingwa wa Africa Tunesia,mjini Cologne.Kufuatia ushindi wa mabao 4-2 wa Argentina dhidi ya Australia siku hiyo hiyo,mutano umepangwa sasa kuania uongozi wa kundi hili .Ushindi wa Ujerumani dhidi ya Tunesia ni wapili katika kombe hili baada ya kwanza kuilaza Australia 4-3.
Sasa Australia na mabingwa wa Afrika Tunesia watakutana kesho kuamua nani habururi mkia katika kundi lao na baadae kufunga virago kurejea nyumbani.
Tunesia itakuwa uwanjani kesho kwa mpambano wao wa mwisho wa Confederations Cup kati yao na Australia kuamua nani hamalizi mkiani mwa kundi lao lililoingiza Argentina ,Australiana Ujerumani.
Kwa Tunesia itakua kujiwinda kurudi Ujerumani mwakani kwa Kombe la dunia,baada ya Morocco inayoongoza kundi lao la 5 kanda ya Afrika kupoteza jana pointi 2 mjini Nairobi walipozimwa na Harambee Stars 0:0 .
Ivory Coast,Ghana,Angola na chipukizi Togo zote zinaweza kuwa timu mpya zitakazopepea bendera ya Africa katika Kombe lijalo la dunia.Ni Tunesia na Morocco tu miongoni mwa timu za kale ambazo zina uhakika moja itakuja Ujerumani.
Stadi wa Chelsea Didier Drogba alitikisa jana wavu mara mbili mjini Abidjan kuitoa Misri nje ya kinyan’ganyiro cha kombe la dunia.Sasa corte d’Ivore iko pointi 2 usoni mwa simba wa nyika Kamerun walioilaza Libya bao 1:0 mjini Dopuala hapo jana.Drogba alipiga hodi katika lango la misri mnamo dakika ya 40 na 49 na kuwafurahisha mashabiki wa nyumbani.Kwa jumla Droga ameshatia mabao 7 katika kinyan’ganyiro hiki cha kanda ya Africa.Sasa Tembo wa I.Coast wanaongoza wakiwa na pointi 19 kwa 17 za simba wa nyika.Tembo watakumbana na simba wa nyika nyumbani mjini Abidjan,Septemba 4 kuamua hatima yao katika Kombe lijalo la dunia.
Kama Afrika kusini, Nigeria ilipatwa na msukosuko nyumbani Lagos, kwani imemudu suluhu tu 1:1 na Angola.Alikuwa nahodha wao J.J.Okocha alieufumania mango wa Angola mnamo dakika ya 5 ya mchezo,lakini waangaloa wakasema hivyo ni vishindo vyenu vya darini vitakavyoishia sakafuni.Kwani, Paulo Figueiredo,alifuta bao la Okocha na sasa ni An gola iliopo kileleni mwa kundi hili huku Nigeria ikifuata nafasi ya pili.
Maajabu yamefanywa na Black Stars-Ghana, ambao wamethubutu kunawiri nyota yao katika anga la Africa Kusini.Ghana iliilaza Bafana bafana mjini Johannesberg mabao 2:0.Mabao yao ya kipindi cha pili yalitiwa na Mathew Amoah na Michael Essien.
Ghana licha ya kuwa mabingwa wa Africa mara 4, hawakuwahi kuteremka katika medani ya kombe la dunia.Kwahivyo, wanadai huu ni mwaka wao.
Chipukizi Togo nao wanaendelea kuzusha maajabu baada ya kumudu suluhu mabao 2:2 na Senegal nyumbani mwao Dakar.Togo sasa ina pointi 17 na ushindi mwengine wa Togo dhidi ya Liberia nyumbani na Kongo, ugenini utawapatia tiketi ya Ujerumani.