1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Dunia la Wanawake 2011

17 Juni 2011

Timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani inalitetea kwa mara ya pili taji la Ubingwa wa dunia kwa wanawake. Mwaka huu ni timu 16 zinazoshiriki kombe la dunia.

https://p.dw.com/p/11dxx
FIFA-Kombe la dunia la wanawake 2011Picha: picture-alliance/augenklick

Nchi ya Ujerumani ndio mwenyeji wa mashindano ya Kombe la dunia la wanawake mwaka huu kuanzia tarehe 26 mwezi huu hadi tarehe 17 mwezi ujao. Hii ni baada ya Ujerumani kushinda haki ya kuwa mwandalizi mnamo mwezi Oktoba mwaka 2007.

Fußball Nationalmannschaft der Frauen WM-Kader
Timu ya taifa ya wanawake UjerumaniPicha: dapd

Katika mashindano ya mwaka huu, ambayo pia ni awamu ya sita kufanyika,Timu 16 zitashindana.Timu ya Ujerumani, ambayo kwa mara ya pili inalitetea taji hilo, ilifuzu moja kwa moja na ilifanikiwa kuchaguwa kundi la mabalozi walioshughulika na wanaoendelea kushughulika na kutoa uhamasisho wa mashindano hayo.

Sharry Reeves ni mmojawapo ya mabalozi hao, ambaye pia ana uzoefu katika ulimwengu wa soka, na ameandika kitabu kuhusu wachezaji wa kike wa soka Ujerumani.

Uhamasisho

Anasema shughuli za kutoa uhamasisho huo bado zinaendelea na wanahimiza watu wanunue tiketi za mashindano hayo.

Na mpaka sasa Sharry anasema mapokezi yamekuwa mazuri, kwa kuwa kiasi ya tiketi laki 7 zimeuzwa ambacho ni kiwango kisicho cha kawaida kwa mashindano ya wanawake. Kiwango ambacho pia kando na Marekani, ambayo iliandaa mashindano hayo mnamo mwaka 1999 na 2003, iliouza kiwango sawa na hicho, hakuna nchi nyengine iliowahi kuuza kiwango hicho cha tiketi.

Mojawapo ya majukumu anayostahili kufanya Sharry miongoni mwa mabalozi wengine wa kombe hilo la dunia ni kuyatumia mashindano hayo kuhimiza mchanganyiko wa makabila na watu wa tabaka mbalimbali, na pia kuimarisha haki za wanawake, na anasema kuwa hili ni suala muhimu mno. Hata hivyo ameeleza kuwa hili halipo nchini Ujerumani, hususan kwenye soka ya wanawake kwa kuwa timu ya taifa na nyenginezo ndogo ambazo zinashirikisha wachezaji wa tamaduni mbali mbali. Hayo Sharry anasema ni mambo yaliokuwepo wakati yeye mwenyewe alikuwa mdogo, lakini halidhihiriki tena.

Akizungumzia maendeleo ya soka la wanawake katika siku za hivi karibuni, Sharry amesema muundo umeimarika zaidi kuliko ilivyokuwa katika siku za nyuma. Na pia mavazi yamekuwa bora. Hili anasema huenda lisitiliwe maanani mno na watu wengi, lakini kutokana na uzoefu wake katika mchezo huo, anasema ni muhimu, maana mavazi ni sehemu inayojenga imani ya mtu.

Changamoto zilizopo

Katika changamoto nyingi zilizopo kwenye mchezo huu kwa wanawake, hususan barani Afrika, ikizingatiwa faida inayodhihirika kwa wachezaji wanawake wa Ulaya, hali ni tofauti kwa wachezaji wa Afrika, hili pia linathibitishwa kutokana na timu za Afrika kwenye mashindano hayo mwaka huu, ambazo ni Equatorial Guinea na Nigeria pekee.

Balozi huyo wa kombe la dunia mwaka huu, amesema timu za Ulaya siku zote huorodheshwa katika nafasi tano za juu ulimwenguni kwa kuwa zina muundo thabiti, na fedha pia. Hili halipo kwa timu za Afrika, na pia kwa timu zinazotoka Marekani kusini, kwa timu kama Brazil, Mexico na timu nyenginezo, fedha huwa ni tatizo kuu.

Frauen Fußballweltmeisterschaft Deutschland - USA
Mpambano wa mwaka 2003 kai ya Marekani na UjerumaniPicha: AP

Na timu hizi hulazimika kujitayarisha dakika za mwisho kabla ya mashindano.

Tatizo jingine alilogusia Reeves ni Muundo ambapo kwa timu za Afrika, mtu anapoziona hahisi kama zinawania taji,na badala yake zinaonekana kuwania kushiriki tu katika mashindano.

Tofuati na timu za Marekani na Ulaya, Reeves anasema timu za Afrika hazijawahi kushinda taji kuu katika historia.


Tunapo tizamia mashindano ya kombe la dunia mwaka huu, huenda ni changamoto basi kwa mataifa mbalimbali barani Afrika, kuimarisha na pia kukuza vipaji katika mchezo huu miongoni mwa wanawake.

Mwandishi: Maryam Abdalla
Mhariri:Miraji Othman