Klose aweka rekodi ya Kombe la Dunia
9 Julai 2014Klose mwenye umri wa miaka 36, ambaye anacheza katika Kombe la Dunia kwa mara yake ya nne, tayari alikuwa ameifikia rekodi iliyowekwa na Ronaldo ya magoli 15 wakati alipofunga goli la kusawazisha katika mchuano waliotoka sare ya 2-2 dhidi ya Ghana katika awamu ya makundi kabla ya kufunga la 16 katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Brazil mjini Belo Horinzonte.
Goli hilo lilikuwa lake la kwanza katika nusu fainali ya Kombe la Dunia na mojawapo ya mabao muhimu kwa sababu liliiweka Ujerumani kifua mbele 2-0.
“sidhani kama ninaweza kupima kile goli hilo linamaanisha kwangu,” alisema Klose, ambaye amesema yeye anafanya kazi yake tu: “mimi ni mshambuliaji na washambuliaji hutaka kufunga magoli. Na kimsingi nataka nisalie kileleni mwa orodha ya wafungaji magoli wengi kwa muda mrefu iwezekanavyo”.
Klose, mwanasoka mtulivu anayechezea klabu ya Lazio baada ya kuanzia Kaiserslautern, Wrder Bremen na Bayern Munich, Klose ndiye mshambuliaji bora wa Ujerumani katika kizazi chake ambaye kiwango chake cha mchezo wa kiutu na maadili yake uwanjani vimewafanya wengi kumuenzi nyumbani Ujerumani na hata nchini Italia.
Alizaliwa nchini Poland na akahamia Ujerumani na familia yake katika mwaka wa 1986 wakati huo akiwa na umri wa miaka minane. Kocha wake Joachim Löw amemmiminia sifa mshambuliaji huyo, akisema kikosi kizima kimefurahishwa na mafanikio ya Klose, na ni mafanikio ambayo alistahili kuyapata.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters