Kiongozi wa upinzani Odinga anataka uchaguzi mpya Kenya
29 Oktoba 2017Idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa Alhamis, ukiwa ni uchaguzi mpya wa rais , baada ya ule uliofanyika mwezi Agosti , inaonesha kwamba mchakato mzima wa uchaguzi ni batili, na serikali ya rais Uhuru Kenyatta inajaribu "kuharibu taasisi nyingine za utawala nchini," ikiwa ni pamoja na mahakama kuu, Odinga amesema. Alisusia uchaguzi , akisema mageuzi ya uchaguzi yanahitajika.
Odinga alizungumza na shirika la habari la AP baada ya makabiliano yaliyosababisha umwagikaji wa damu kati ya polisi na waungaji mkono wa upande wa upinzani katika baadhi ya sehemu za Kenya tangu uchaguzi huo kufanyika, pamoja na kuahirishwa kwa uchaguzi katika maeneo ambayo ni ngome kuu za upinzani ambako vituo vya kupigia kura havikuweza kufunguliwa kwasababu ya matatizo ya kiusalama.
Mahakama kuu ilibatilisha uchaguzi wa hapo Agosti 8, baada ya kugundua kile ilichosema kuwa ni mapungufu na kutokuwa na uhalali, na kusababisha ukosoaji mkali kutoka kwa rais Kenyatta, ambaye alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
"Nchi yetu imo katika hatari kubwa," amesema Odinga, licha kukiri kuwa tayari kwa majadiliano na kambi ya Kenyatta juu ya kufanyika kile alichokiita uchaguzi huru na wa haki.
"Sisi sio kwamba hatuko tayari kwa mazungumzo lakini ajenda bado itakuwa ile ile , jinsi gani ya kuweka uwanja sawa ili uchaguzi uweze kufanyika katika muda wa siku 90," Odinga alisema katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake mjini Nairobi. " Hiki ndio tutakuwa tayari kukijadili na wao."
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali kutoka vituo vya kupigia kura ambayo yamewekwa katika tovuti ya tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya yanaonesha kwamba Kenyatta amepata kura nyingi katika maeneo mengi baada ya uchaguzi wa hapo Alhamis. "Kimsingi ilikuwa Uhuru dhidi ya Uhuru," Odinga amesema.
Wakati huo huo mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati alitarajiwa kutangaza leo iwapo uchaguzi utaendelea katika maeneo yaliyozuka ghasia ya upinzani, ambako ususiaji umezusha maandamano ya ghasia katika uchaguzi ambao unatarajiwa kumpa Uhuru Kenyatta ushindi wa kishindo , lakini wenye dorasi.
Wakati zoezi la kuhesabu kura likiwa karibu limekamilika baada ya uchaguzi wa hapo Alhamis , matokeo bado hayajatangazwa rasmi wakati maafisa wakitafakari kile cha kufanya juu ya majimbo 25 ya kupiga kura ambako uchaguzi ulizuiwa.
Katika maeneo hayo, waungaji mkono wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga walifanikiwa kuzuwia mamia ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa, na kusababisha makabiliano ya vurugu na polisi ambayo yaliendelea kwa siku kadhaa, na kusababisha watu tisa kuuwawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Kiasi ya watu 49 wameuwawa tangu uchaguzi wa kwanza wa rais Agosti 8, ambao baadaye ulibatilishwa, na kusababisha mzozo mkubwa wa kisiasa nchini Kenya katika muongo mmoja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Yusra Buwayhid