1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KIGALI : Tume kuchunguza Ufaransa na mauaji ya halaiki

5 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFZd

Wabunge wa Rwanda wameidhinisha kuanzishwa kwa tume ya uchunguzi kuangalia madai ya kuhusika kwa Ufaransa katika mauaji ya halaiki yaliopelekea kuuwawa kwa watu 800,000 katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati muongo mmoja uliopita.

Bunge limepitisha sheria Jumanne iliopita juu ya kuanzishwa kwa tume hiyo.

Jopo hilo litachunguza dhima ya Ufaransa katika mauaji hayo ya siku 100 ambayo yaliandaliwa na kutekelezwa na serikali iliokuwa ikihodhiwa na kabila la Wahutu na ambayo ilikuwa ikiungwa mkono na serikali ya Ufaransa.

Ufaransa mara kwa mara imekuwa ikishutumiwa na serikali ya sasa ya Rwanda inayodhibitiwa na Watutsi kwa kuwafunza na kuwapatia silaha wale waliohusika na mauaji hayo madai ambayo yanakanushwa na serikali ya Ufaransa.