1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya sheria ya vyama vya siasa yaanza kusikizwa Tanzania

George Njogopa4 Januari 2019

Mahakama nchini Tanzania imeanza kusikiliza kesi inayopinga mswada wa sheria ya vyama vya siasa. Viongozi wa vyama vya siasa wanaupinga mswada huo wakisema unakiuka katiba.

https://p.dw.com/p/3B2r7
Joran Bashange, Zitto Kabwe und Salim Abdalla Biman
Picha: DW/Said Khamis

Mahakama Kuu ya Tanzania leo imeanza kusikiliza kesi iliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya siasa wakipinga sheria ya vyama vya siasa kutowasilishwa kwa mara ya pili bungeni wakidai unakiuka katiba ya nchi na mahakama hiyo imetoa muda wa siku saba kwa serikali kujitetea. 

Kesi hiyo ambayo imefunguliwa na kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe na wenzake watatu, kutoka vyama vya CUF na CHAUMA, ilibidi isubiri hadi muda wa mchana kutolewa maamuzi baada ya kushuhudia wanasheria wa pande zote mbili wakichuana kwa hoja nyakati za asubuhi wakati aliposomwa kwa mara ya kwanza.

Akitoa uamuzi huo wa awali, kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Barke Sahel alitupilia mbali maombi ya mwanasheria wa serikali aliyetaka apewa muda wa siku 21 kuwasilisha utetezi wake na badala yake akamuamuru kuwasilisha utetezi huo ndani ya siku saba.

Katika maelezo yake, Jaji Sahel alisema kuwa vile shauri hilo limewasilishwa kwa hati ya dharura na kwamba lina maslahi ya umma na kwa kuzingatia kwamba muswada huo unaolalamikiwa umepangwa kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza Januari 15, hivyo mjibu maombi anapaswa kuwasilishwa utetezi wake kabla ya Januari 9.

Wanaotaka mswada huo utupiliwe mbali wanasema kuwa umetawaliwa na mapungufu mengi
Wanaotaka mswada huo utupiliwe mbali wanasema kuwa umetawaliwa na mapungufu mengiPicha: DW/Said Khamis

Katika kesi yao ya msingi, waombaji hao wanapinga sheria mpya ya vyama vya siasa ambayo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni wakisema kuwa imetawaliwa na mapungufu mengi.

Miongoni mwa hoja zao ni pamoja na ile wanayodai kuwa iwapo sharia hiyo itapitishwa itakuwa imempa mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa ikiwamo yale yanayohusu uongozi.

Tangu kuletwa kwa sheria hiyo mpya ya vyama vya siasa, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wapinzani na hivi karibuni waliunda umoja wao unaoundwa na vyama kumi wakiazimia mambo mbalimbali pamoja na kutumia mikono ya sheria kuipinga

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef