1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya mauwaji ya TerreBlanche yafunguliwa Afrika Kusini

Oumilkher Hamidou6 Aprili 2010

Hali ni tete karibu na jumba la mahakama inakosikilizwa kesi ya vijana wawili weusi wanaosemekana kumuuwa kiongozi wa kibaguzi TerreBlanche

https://p.dw.com/p/Mo6Z
Kiongozi wa chama cha kibaguzi cha AWB Eugene TerreBlanche(kati kati)Picha: AP

Mamia ya waafrika kusini,kuanzia wazungu wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia mpaka kufikia waafrika kusini weusi wanaoishi katika maeneo ya karibu, wamekusanyika karibu na korti ya Ventersdorp,kaskazini magharibi ya Afrika kusini,kusikiliza kesi dhidi ya vijana wawili wanaotuhumiwa kumuuwa kiongozi wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia,Eugene Terre'Blanche.

Ili kuepusha vurumai na fujo,idadi kubwa ya polisi wamewekwa karibu na jengo la mahakama ambako watuhumiwa hao walikuwa wafikishwe tangu leo asubuhi.

Polisi wamezungusha senyenge katika jengo lote la mahakama ili kuwazuwia mashawishi wasilijongelee.Kesi hiyo ni ya siri kwakua mmojawapo wa watuhumiwa bado ni mdogo.

Licha ya mvua na idadi kubwa ya polisi,mashawishi wamesimama kwa makundi mawili yanayopeana uso.

Kwa upande mmoja kuna wafuasi wa chama cha makaburu cha AWB kilichoundwa na Euegene TerreBlanche,wakivalia mashati ya rangi ya kaki yenye nembo ya chama chao inayofanana na ile ya utawala wa zamani wa wanazi.

Upande wa pili wanakutikana baadhi ya waafrika kusini weusi waliovalia fulana za chama tawala cha ANC na nyengine zenye picha ya rais Jacob Zuma.

Licha ya kutenganishwa na polisi kila upande unaunyooshea kidole upande wa pili.

Wafuasi wa AWB wanaimba nyimbo za enzi za zamani za ubagizi wa rangi na mtengano-Apartheid na kuwafanya wapinzani wao wa upande wa pili wajibishe kwa kuimba Nkosi Sikeleli Afrika-Mungu ibariki Afrika-wimbo wa taifa ulioanzishwa baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mnamo mwaka 1994 nchini Afrika kusini.

Süsafrika Jacob Zuma nach der Wahl
Rais Jacob Zuma wa Afrika KusiniPicha: AP

Viongozi wa Afrika kusini,ikiwa ni pamoja na rais Jacob Zuma,tangu jumamosi iliyopita wanaendelea kuwatolea amwito wananchi wawe watulivu.

Msemaji wa chama cha AWB Pieter Steyn ameliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba wametoa mwito wa kuwepo hali ya utulivu na wanataraji wanachama wao wataheshimu mwito huo na hawatajihusisha na visa vya matumizi ya nguvu.

Eugene Terre'Blanche,ambae chama chake cha siasa kali za mrengo wa kulia AWB kilifanya njama kadhaa za mauwaji mapema miaka ya 90 kutaka kuzuwia mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano-Apartheid usipigwe marufuku,amekutikana ameuwawa jumamosi iliyopita akiwa nyumbani katika shamba lake huko Ventersdorp-umbali wa kilomita kama mia moja hivi magharibi ya Johannesburg.

Wawili kati ya wakulima wake ,mmoja akiwa na umri wa miaka 15 na wa pili miaka 28 wamejisalimisha moja kwa moja kwa polisi.Wamesema walizozana na muajiri wao kwasababu ya malipo ya mshahara yao.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/Reuters

Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman