1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: IEBC kuongeza kasi ya kuhakiki matokeo

13 Agosti 2022

Tume ya IEBC nchini Kenya imeiongeza kasi ya kuhakiki matokeo ya uchaguzi wa rais kutokea maeneo bunge ili kuhitimisha kazi yake katika muda wa siku saba ilizopewa kikatiba.

https://p.dw.com/p/4FU9Q
Ballot boxes and voting materials at Nyali polling station in Mombasa
Picha: Halima Gongo/DW

Kufikia sasa fomu 43 kati ya zote 290 za matokeo ya maeneo bunge zimethibitishwa. Wakati huo huo afisa msimamizi wa IEBC kutokea kituo cha Embakasi East hajulikani haliko. Kadhalika idadi ya wanawake waliochaguliwa kuwa magavana imeongezeka hadi 6 mpaka sasa.

soma Shughuli ya kuhesabu kura za Wakenya inaendelea

Tume ya uchaguzi IEBC imeiongeza kasi ya kuhakiki fomu za 34B kutokea maeneo bunge yote 290. Kwa sasa idadi ya madawati ya uhakiki yameongezwa na kufikia 12 kutokea matano. Kimsingi kila fomu inafanyiwa tathmini katika muda wa dakika 40.Maafisa wote 290 wasimamizi wa IEBC wako kwenye kituo cha Bomas of Kenya cha kujumlisha matokeo ya kitaifa kuwasilisha fomu za 34B za maeneo bunge.Saa chache zilizopita zilizuka purukushani kati ya mawakala wa Azimio la Umoja One Kenya na Kenya Kwanza pale mwakilishi wa wanawake Gladys Shollei alipoonekana akibeba karatasi ambazo hazikueleweka.Hii ni mara ya pili kwa mtafaruku kama huo kutokea ukumbini Bomas.

soma Chama cha UDA cha taraji ushawishi mkubwa bungeni Kenya

Afisa msimamizi wa IEBC aripotiwa kupotea

Kenia Wahlen
Mwenyekiti wa IEBC Wafula ChebukatiPicha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Yote hayo yakiendelea, afisa msimamizi wa IEBC kutokea kituo cha Embakasi East hajulikani aliko. Kulingana na mwenyekiti wa tume, Wafula Chebukati, Daniel Musyoka alipotea tangu siku ya Alhamisi.

"Tayari ripoti ya mtu aliyepotea imewasilishwa kwa polisi.' Alisema Chebukati.

Daniel Musyoka alikuwa akihudumu kwenye kituo cha East African School of Aviation cha kuhesabia kura.Tayari ripoti ya mtu aliyepotea imewasilishwa kwa polisi. Tukio hilo lilizua vurugu hapo Bomas.

soma Madai ya wizi wa kura yazusha malumbano Nairobi

Wakati huohuo, afisa mkuu mtendaji wa tume ya IEBC Hussein Marjan ameweka bayana kuwa visa 200 vya kuingilia mfumo wao elektroniki na mtandao vimeripotiwa.

"Tunajua watu hawali, wanataka kuhakikisha kwamba mifumo yetu ya teknologia inateteleka. Lakini niwaambie kuwa haiwezekani tumejiandaa vizuri" alisema Marjan.

IEBC imesisitiza kuwa mikakati yao ni thabiti na kwamba uwezekano wa kuingilia na kuvuruga mitambo yao haupo.

Wanawake watamba

Kenia Nairobi Wahlen Wahllokal
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa upande mwengine, kwa mara ya kwanza katika historia ya ugatuzi, idadi ya magavana wanawake imeongezeka baada ya uchaguzi mkuu huu.Kwa sasa wanawake wasiopungua 6 wamenyakua nafasi za kuwa magavana wa kaunti za Meru,Kirinyaga,Homa Bay,Nakuru na Kwale.Fatma Achani ndiye gavana mpya wa kaunti ya Kwale.

"Ushindi wangu ni ushindi wetu sote, nataka tu niwaulize wale Wakwale wote haijalishi ulipigia nani kura, ulipigia gavana nani kura sasa hivi nyote gavana wenu ni Fatu,a Achani."

Tume ya IEBC ina muda hadi tarehe 16 Agosti kuyatangaza matokeo ya mshindi wa kinyanganyiro cha urais.

 

Thelma Mwadzaya, DW  Nairobi